Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuandaa mikakati endelevu ya kuimarisha na kusimamia maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye bila kuathiri utoaji wa huduma za Serikali.
Dkt. Yonazi ametoa wito jijini Dodoma, wakati wa kikao cha kupitia na kuimarisha usimamizi, ujenzi na uendeshaji wa Mji wa Serikali, ambapo ameupongeza Wakala wa Majengo Tanzania kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutumia mifumo ya kisasa katika kusimamia uendelezaji wa mji huo.
Amesema kuwa kutokana na umuhimu wa Mji wa Serikali katika kurahisisha shughuli za kiutawala na utoaji wa huduma kwa wananchi, ni muhimu TBA kuweka mipango inayozingatia ukuaji wa mahitaji ya Serikali pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza kadri mji huo unavyoendelea kupanuka.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na uendeshaji ili kuhakikisha miundombinu na majengo ya Serikali yanatunzwa na kuendelea kuwa katika hali nzuri kwa matumizi ya muda mrefu.
Ameeleza kuwa mipango endelevu inapaswa kuwa msingi wa kuhakikisha Mji wa Serikali unaendelea kukua kwa utaratibu, huku ukitoa mazingira bora ya kufanyia kazi kwa watumishi wa umma na kuwezesha wananchi kupata huduma za Serikali kwa ufanisi.





