• Hukumu ya Mahakama Kuu yagawanya walimu, wazazi kuhusu nidhamu shuleni
  • Wadau wataka Wizara ya Elimu kuweka mwongozo wa adhabu mbadala
  • UNICEF, asasi zaidi ya 20 zaunga mkono uamuzi, zasisitiza malezi bila vipigo

Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Zuio la adhabu ya viboko shuleni limewagawa walimu na wazazi, baadhi wakiunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu na wengine wakihofia kuporomoka kwa nidhamu; imefahamika.

Kwa miaka mingi, fimbo imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kusimamia nidhamu shuleni, lakini sasa Mahakama Kuu imebatilisha kanuni zilizoruhusu matumizi yake.

Wakati baadhi ya wadau wakieleza kuwa uamuzi huo utasaidia kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na madhara ya kimwili na kisaikolojia, wengine wameonya kuwa kuondoa viboko bila kuweka mfumo mbadala kutaongeza changamoto za nidhamu.

Mjadala huo umeibuka kufuatia hukumu ya Novemba 3, 2026, iliyotolewa na Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma, katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Samwel Maduhu dhidi ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jopo la majaji watatu, Amiri Mruma, Suleiman Hassan na Irene Musokwa, lilibaini kuwa kanuni zilizoruhusu wanafunzi kuadhibiwa kwa viboko zilikinzana na haki za kikatiba zinazolinda utu wa binadamu na kuzuia adhabu ya kikatili au inayodhalilisha.

Mahakama ilibatilisha Kanuni ya 3 ya Kanuni za Elimu kuhusu Adhabu ya Viboko za mwaka 2002, ikisomwa pamoja na tafsiri ya adhabu hiyo katika Kanuni ya 2, na sehemu ya Kanuni ya 6 iliyoruhusu mwanafunzi kuondolewa shuleni kwa kukataa kuchapwa.

Uamuzi huo ulianza kutumika mara moja, lakini haukuondoa mamlaka ya shule kusimamia nidhamu kwa kutumia hatua nyingine zinazokubalika kisheria.

Walimu wagawanyika

Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gema Akilimali, ambaye pia amewahi kuwa mwalimu, amesema anaunga mkono juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya vipigo, lakini Wizara ya Elimu inapaswa kutoa mwongozo wa namna ya kurekebisha tabia za wanafunzi.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 24 – 30, 2026