- Rais achora ramani kuelekea kupata Katiba mpya 2028/2029, Tume ya Maridhiano
- Dk. Bana ataka CHADEMA, ACT Wazalendo kushirikishwa, akisisitiza kutowapuuza
- Dk. Chegeni ashauri vyama kukaa mezani, Anna Henga aonya mchakato usiharakishwe
Na Waandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Matumaini ya kupata Katiba mpya yamerejea baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza mwelekeo wa maridhiano ya kitaifa na ratiba ya mabadiliko ya Katiba; JAMHURI linaripoti.
Kauli ya Rais kwamba Tanzania itakuwa na Katiba iliyorekebishwa au mpya ifikapo mwaka 2028 au 2029, imefungua mjadala kuhusu hatua zinazohitajika kutimiza ahadi hiyo, baada ya mchakato wa Katiba kukwama kwa miaka mingi.
Katika mazungumzo maalumu na JAMHURI, wanasiasa, wasomi na watetezi wa haki za binadamu wamekaribisha mwelekeo huo kwa moyo mkunjufu, wakisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji mpana, ratiba inayoeleweka na kuondoa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha maridhiano.
Miongoni mwa hoja zinazojitokeza ni kutokuwapo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mazungumzo ya sasa, huku Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, akiwa gerezani.
Rais Samia alitoa kauli hiyo Novemba 20, mwaka huu, katika mkutano wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika Shule ya Polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema serikali inaendelea na maandalizi ya Tume ya Maridhiano, ikiwa imefanya mashauriano na vyama vya siasa, taasisi za kiraia na viongozi wa dini kuhusu uwakilishi.
Alieleza kuwa mashirika ya dini yameombwa kuwasilisha majina ya watu watakaoshiriki katika Tume, akirejea ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuhusu mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo imeongeza matarajio kwamba suala la Katiba, ambalo limekuwa sehemu ya madai ya mabadiliko ya kisiasa kwa muda mrefu, sasa linaingia hatua za utekelezaji.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 24 – 30, 2026


