*Waugeuza kuwa uwanja wa vita, askari wa TFS, wahifadhi wajeruhiwa, Serikali yakunjua makucha

*Pikipiki 5 za Serikali zachomwa moto; waharibu hekta 400, mikarambati yachomwa mkaa

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Handeni

Watu 10 wakiwamo askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na walinzi wa misitu katika vijiji, wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na kundi la watu waliokuwa na mapanga, sime na marungu ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Nishati Korogwe wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Kati yao, askari wawili, MG Geofrey Muro na SR2 Noel Abraham, hali zao ni mbaya kutokana na kukatwa vibaya na majahili hao waliovamia hifadhi.

Katika tukio hilo lililotokea wakati askari walipokuwa wakifanya doria ya kawaida, pikipiki tano mali ya Serikali zilichomwa moto. Askari mmoja aliokotwa usiku wa manane baada ya kujikongoja kwa muda mrefu ndani ya msitu, huku mwenzake akipatikana alfajiri ya siku iliyofuata, akiwa amejeruhiwa vibaya.

Haya yametokea wakati mamia ya wafugaji wakiwa wameingia msituni na kujenga maboma ya mifugo, kuchoma mkaa na kufanya shughuli nyingine zinazokiuka masharti ya uhifadhi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese aliyezungumza na JAMHURI ofisini kwake mwishoni mwa wiki, askari hao hawakuwa na silaha kwa kuwa walikuwa kwenye doria ya kawaida.

“Askari wetu walikuwa wanafanya doria za kawaida. Kwa sababu msitu wetu hauna wanyama wakali, tuliona hakuna haja ya kuwa na silaha kwenye doria hizo. Walikuwa na pikipiki kwenda kufanya doria,” amesema Nyamwese.

Anasema wakati askari hao walipowakuta baadhi ya wavamizi hao wakichoma mkaa, walipojaribu kuwauliza kuhusu shughuli hizo, hali ilibadilika ghafla, wakajikusanya na kuwashambulia.

“Walitumia silaha zao za asili, sime walizokuwa nazo na zile fimbo, wakaanza kuwashambulia askari wetu. Wawili walipigwa vibaya mno,” anasema Mkuu wa Wilaya.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 24 – 30, 2026