WASHINGTON, MAREKANI
Utafiti mpya wa Kituo cha Utafiti cha Pew unasema kufikia mwaka 2035, Waislamu wataongezeka na kufikia bilioni 2.57 na Wakristo watakuwa bilioni 2.52 duniani kote.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa wiki iliyopita yanasema watafiti wanahusisha mabadiliko hayo na kasi ya ongezeko la viwango vya uzazi.
Pew inasema ingawa idadi ya waumini wa dini zote mbili inaongezeka, idadi ya Waislamu inakua kwa kasi zaidi huku sababu kuu ni kwamba kwa wastani wanapata watoto wengi zaidi kuliko waumini wa makundi mengine makubwa ya kidini.
Mtaalamu Mwandamizi wa Demografia wa Pew, Conrad Hackett, amesema sababu kubwa ni watoto wanaozaliwa.
Makadirio yaliyotolewa yanaonyesha kati ya mwaka 2020 na 2025, wanawake Waislamu walikuwa na wastani wa watoto 3.1, ikilinganishwa na watoto 2.5 kwa wanawake Wakristo.
Kwa wanawake wa makundi mengine yote kwa pamoja, wastani ulikuwa watoto 1.6, chini ya kiwango cha takriban watoto 2.1 kinachohitajika kudumisha idadi ya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Pia kwa makadirio ya kituo hicho, mwaka 2020 kulikuwa na Wakristo bilioni 2.27 na Waislamu bilioni 2.02 duniani.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 24 – 30, 2026

