*Milya asema uongozi wa Rais Samia umefungua milango ya uwekezaji, utalii

Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TANZANIA imeendelea kujijengea nafasi ya kimataifa katika masuala ya afya ya mama na mtoto huku nchi mbalimbali za Afrika zikianza kuitazama kama mfano wa kuigwa kutokana na hatua zinazochukuliwa kuboresha huduma za afya, kupunguza vifo vya uzazi na kuimarisha mifumo ya huduma za dharura.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Kinyasi Milya wakati akielezea matokeo ya ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Ethiopia.

Milya amesema ziara hizo zimekuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kufungua fursa za kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.

Anasema ziara ya Uganda iliyofanyika Novemba 18 hadi 19 mwaka huu ililenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda kupitia mazungumzo ya Rais Samia na mwenyeji wake Rais Yoweri Kaguta Museveni.

Ameeleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Uganda umejengwa kwa muda mrefu tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kuendelea kuimarishwa na viongozi waliofuata akiwamo Rais Samia.

Anasema, mahusiano hayo yameendelea kuwa na mchango mkubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambako Tanzania imeendelea kushirikiana na nchi wanachama katika masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya kikanda.

Amesema katika ziara hiyo viongozi wa Tanzania na Uganda walikubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ili kuwawezesha wananchi kutumia fursa zinazotokana na ujirani na ushirikiano wao.

Akizungumzia ziara ya Ethiopia Milya alisema uteuzi wa Rais Samia kuwa kinara wa Umoja wa Afrika katika masuala ya afya ya mama na mtoto ni fursa muhimu kwa Tanzania kuimarisha ushawishi wake wa kimataifa na kuonesha mchango wake katika kuboresha afya ya wananchi.

Amesema nafasi hiyo imepata uzito zaidi kupitia uzinduzi wa mpango elekezi wa kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026).

Ameeleza kuwa mkutano huo ulitarajiwa kuhudhuriwa na washiriki 30,000 lakini idadi iliongezeka hadi kufikia takribani 42,000 jambo linaonesha mwitikio mkubwa wa washiriki baada ya kutangazwa kuwa Rais Samia angezindua mpango huo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bakari Machumu ameeleza kuwa mpango huo unahusisha nchi zote 55 za Umoja wa Afrika na umejengwa katika malengo makuu matatu yanayojulikana kama ‘Sifuri Tatu’.

Lengo la kwanza ni kuhakikisha hakuna mama anayejifungulia nyumbani bila uangalizi wa wataalamu wa afya kwa kuhamasisha wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya vinavyotoa huduma salama.

Lengo la pili ni kutokomeza vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika kupitia uboreshaji wa huduma za afya, huku lengo la tatu likiwa ni kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo muhimu zinazolinda afya na maisha yake.

Machumu alisema umuhimu wa mpango huo unatokana na hali ya vifo vya uzazi na watoto wachanga barani Afrika, huku takwimu za mwaka 2023 zinaonesha takribani wanawake 180,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi huku watoto wachanga milioni 1.18 wakipoteza maisha.

Amesema mpango huo si ajenda ya afya pekee, bali ni sehemu ya juhudi za kulinda maisha ya wananchi, kujenga nguvu kazi yenye afya na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.

Amefafanua kuwa katika uzinduzi huo Rais Samia alitangaza hatua mbili muhimu, ikiwamo kutoa nafasi 60 za ufadhili wa mafunzo ya ubobezi kwa wataalamu wa afya barani Afrika, hususan katika fani za ukunga, ganzi, afya ya uzazi na huduma za watoto wachanga.

Hatua nyingine ni kuimarisha mfumo wa uwajibikaji kwa kutumia viashiria saba vitakavyosaidia kupima maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha ahadi zinazotolewa na viongozi zinabadilika kuwa matokeo yanayopimika.

Ameeleza kuwa takwimu za Tanzania Demographic and Health Survey za mwaka 2015/2016 zilionesha vifo vya uzazi 556 kwa kila vizazi hai 100,000 idadi iliyoshuka hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 katika takwimu za mwaka 2022.

Amesema Rais Samia alieleza katika mkutano wa Addis Ababa kuwa kiwango hicho kinaonesha dalili za kushuka zaidi hadi takribani 75 kwa kila vizazi hai 100,000, huku akibainisha kuwa taarifa rasmi zinatarajiwa kuthibitisha kiwango hicho.

Akizungumzia faida za nafasi ya Tanzania katika uongozi wa afya ya mama na mtoto, Milya alisema hatua hiyo inaongeza heshima ya nchi, kuimarisha ushawishi wake wa kimataifa na kufungua fursa za kupata ushirikiano kutoka kwa mashirika ya maendeleo.

Tanzania imeanza kuwa mfano wa kujifunza kwa nchi nyingine za Afrika kutokana na ubunifu na mifumo inayotumika kuboresha huduma za afya, akitolea mfano mfumo wa M-Mama unaotumia teknolojia ya kidijitali kurahisisha usafiri wa dharura kwa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.

Amesema nchi za Lesotho, Malawi na Kenya zimekuwa zikija Tanzania kujifunza mfumo huo ili kuona namna ya kuutumia katika kuboresha huduma za afya katika nchi zao.

Aidha alisema nafasi hiyo inaweza kuongeza fursa za kuvutia wawekezaji katika viwanda vya dawa na vifaa tiba, kutokana na Tanzania kupata nafasi ya kujitangaza katika mikutano mikubwa ya kimataifa inayohusisha sekta ya afya.

Amesema viongozi, wataalamu na wageni wanaokuja nchini kwa ajili ya mikutano ya afya au kujifunza mifumo ya huduma wanaweza kutumia nafasi hiyo kutembelea vivutio vya utalii kama Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Zanzibar.

Ametaja matumizi ya huduma za usafirishaji, ikiwamo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kuwa sehemu ya fursa zinazoweza kunufaisha sekta nyingine za uchumi.

Katika eneo la teknolojia, alisema uongozi huo unatoa msukumo kwa vijana na kampuni changa za ndani kubuni mifumo ya kidijitali inayoweza kuboresha utoaji wa huduma za afya, huku ikifungua fursa za kupata mitaji na masoko ya kimataifa.

Amesema pia hadhi inayojengwa na Tanzania katika sekta ya afya inaweza kuongeza nafasi ya nchi kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa, hatua itakayoongeza idadi ya wageni na kuchochea shughuli za kiuchumi katika miji kama Dar es Salaam, Arusha, Zanzibar na Dodoma.