RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Mpango wa Taifa wa Kuboresha Huduma za Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana wa mwaka 2026–2030, unaolenga kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na vya watoto pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Dkt. Samia amezindua mpango huo Novemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe (RMNCAH+N).

Katika mkutano huo, Rais pia amezindua Taarifa ya Hali ya Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Watoto chini ya Miaka Mitano ya mwaka 2026, inayoonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua hadi kufikia 76 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto wachanga vikifikia 17 na vya watoto chini ya miaka mitano vikiwa 28 kwa kila vizazi hai 1,000.

Akizungumzia mafanikio hayo, Dkt. Samia amesema Tanzania inalenga kufikia malengo ya tatu ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030, ambayo ni kupunguza vifo vya uzazi hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto wachanga hadi 12 na vya watoto chini ya miaka mitano hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma bora za afya ya mama na mtoto zinawafikia wanawake na watoto wote kulingana na mahitaji yao, hususan katika maeneo yenye upungufu wa huduma hizo.

“Huduma bora za mama na mtoto zinapaswa kuwafikia wanawake wote na watoto kulingana na mahitaji yao, hasa katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa huduma hizi,” amesema.

Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia mikataba ya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana, inayolenga kuunga mkono ajenda ya Sifuri Tatu inayohimiza kujifungulia katika vituo vya afya, kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya umeongeza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi, ambapo zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania sasa wanapata huduma za afya ndani ya kilomita tano kutoka wanapoishi.

Katika hatua nyingine, amesema vituo maalumu vya kuhudumia watoto wachanga vimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025, huku mfumo wa rufaa wa m-Mama ukiwa umesaidia kusafirisha wagonjwa zaidi ya 250,000, wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto wachanga.

Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo unahitaji ushirikiano wa Serikali, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo, sambamba na upatikanaji wa ufadhili endelevu na kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji huduma za afya.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa mipango ya afya na lishe katika ngazi zote ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.“Mipango ya lishe inafanyiwa tathmini mara kwa mara, huku akibainisha kuwa hivi karibuni Wakuu wa Mikoa walikutana jijini Dodoma kwa ajili ya tathmini ya lishe na kupitia mkataba mpya wa makubaliano uliosainiwa leo, unaolenga kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango hiyo.”amesema Mchengerwa

Aidha, Mhe.Mchengerwa amesema Serikali imeimarisha utaratibu wa mapitio ya vifo vya mama na watoto wachanga, ambapo tathmini hufanyika kila siku katika ngazi za halmashauri na mikoa, huku kila kifo kinachotokea nchini kikijadiliwa kitaifa kwa njia ya mtandao ili kubaini visababishi na kuweka hatua za kuzuia vifo vingine. Ameongeza kuwa huduma za watoto wachanga zimeendelea kuimarishwa ili kuboresha matokeo ya huduma za afya.

Katika eneo la takwimu, Mhe. Mchengerwa amesema kwa muda mrefu nchi imekuwa ikitegemea tafiti za kitaifa (surveys) kufahamu viwango vya vifo, ambapo takwimu za mwisho zilizotangazwa zilitokana na Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS-MIS) wa mwaka 2022.

Hata hivyo, mwaka huu wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi za Mtakwimu Mkuu wa Serikali Tanzania Bara na Zanzibar, NIMR, ZAHRI, Chuo Kikuu cha Dodoma na MUHAS wamechambua takwimu za mifumo ya ndani ya afya ili kukokoto.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe amesema wadau wa sekta ya afya nchini wanatakiwa kuunganisha nguvu na kuongeza ushirikiano katika kuboresha afya na ustawi wa mama, mtoto, vijana na makundi mengine ya jamii ili kuinua ubora wa maisha ya wananchi.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkutano huu ni fursa muhimu kwa viongozi, wataalamu wa afya na wadau kutoka taasisi mbalimbali kukutana, kujadili masuala yanayohusu afya ya jamii na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuimarisha huduma na ustawi wa wananchi,” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa mkutano huo umekutanisha takribani washiriki 1,300 wakiwemo wataalamu wa afya wanaotoa huduma katika taasisi na maeneo mbalimbali nchini, akiwataja kuwa sehemu muhimu ya nguvu kazi inayobeba jukumu la kuimarisha sekta ya afya.

Pia, amesema pamoja na washiriki kuwa na majukumu mengi, ushiriki wao unaonesha dhamira ya pamoja katika kuhakikisha masuala ya afya ya uzazi, mama, mtoto, vijana na lishe yanapewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya afya.