Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameitaka Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) itumie ujuzi iliyoupata kwenye mafunzo ya uongozi kuwa wabunifu zaidi na kuibua vyanzo vipya vya mapato vitakavyoongeza mapato ya shirika hilo na ya Taifa kwa ujumla.
Bw. Mchechu alitoa wito huo Ijumaa, Novemba 27, 2026, jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya uongozi na utulivu kwa menejimenti ya TANAPA, yaliyoanza Novemba 23 na kuendeshwa na Chuo cha Utumishi wa Umma.
Mbali na suala la mapato, aliwataka viongozi hao waandae utaratibu wa kutathmini mchango wa mafunzo hayo katika kuongeza tija kiutendaji.
Aidha, aliwataka wahakikishe watendaji walio chini yao nao wanapata mafunzo ya aina hiyo ili wote wazungumze lugha moja na kuleta tija bora zaidi katika uendeshaji wa Shirika.
Vilevile, aliwataka watumie mafunzo hayo kuweka mikakati imara ya kutekeleza Dira 2050.
Bw. Mchechu aliwasihi pia wajijengee utaratibu wa kusoma vitabu na maandiko yanayoimarisha vipaji vya uongozi ili waendelee kuwa viongozi imara na kutenda haki kwa walio chini yao wakati wote. Aliwataka pia watenge muda wa kufanya mazoezi ya viungo, akisema mazoezi ni jambo muhimu kwa afya ya kiongozi.
Aliipongeza menejimenti ya TANAPA, chini ya Kamishna wa Uhifadhi Massana Mwishawa, kwa kutenga fedha na muda wa kufanikisha mafunzo hayo, akisema taasisi nyingi hutamani kuandaa vipindi vya namna hiyo lakini hushindwa kuvitekeleza.
“Kupanga ni jambo moja na kutekeleza ni jambo lingine. Kwenu ninyi TANAPA mmeweza kupanga na kutekeleza kufanya mafunzo haya muhimu,” alisema.
Mafunzo yalihusisha mada 12, zikiwemo uongozi, maadili na uwajibikaji; stratejia za uongozi kwenye sekta ya umma; akili hisia na uongozi binafsi; udhibiti wa msongo wa mawazo na afya ya akili; tathmini ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na kanuni zake za mwaka 2022; pamoja na itifaki za kijeshi.



