Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwandishi maarufu wa riwaya Afrika, Mnigeria Chinua Achebe, alipata kuandika sentensi maarufu katika kujenga mshikamano wa kijamii kuwa: “Katika mtanziko wa hatari, tumfukuze mbwa mwitu kwanza, kisha tumzuie mwanambuzi kuchezea vichakani.” Sitanii, kichwa cha makala hii kinaweza kuonekana kimekuwa kirefu kuliko kawaida, ila kina maana.
Baada ya matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 kutokana na Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania, taifa letu limejikuta katika kipindi kigumu cha kujitafakari.
Haya si matukio ya kubezwa wala kupuuzwa. Ni alama kwamba kuna jambo haliko sawa katika misingi yetu ya kisiasa, kijamii na hata kiutamaduni. Ni wakati wa kujiuliza maswali magumu – bila woga, bila upendeleo.
Ujio wa aliyekuwa Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, kwa mwaliko wa Umoja wa Mataifa kuchunguza na kushauri juu ya hali hiyo, ni ishara tosha kwamba suala hili lina uzito wa kimataifa.
Hata hivyo, suluhisho la kweli halitatoka nje ya mipaka yetu kama sisi wenyewe hatuko tayari kubadilika. Hapa ndipo hekima ya methali inapopata nguvu kwamba: “Tufukuze mbwa mwitu kwanza, kisha tumzuie mwanambuzi kuchezea vichakani.”
Sitanii, mbwa mwitu katika muktadha huu ni vurugu, chuki za kisiasa, na mifumo dhaifu inayoruhusu tofauti za kisiasa kugeuka uhasama.
Ni tabia ya kushindwa kukubali matokeo, au kushindwa kusikiliza malalamiko ya haki. Ni matumizi ya lugha kali kutoka kila upande, propaganda na vitendo vinavyovunja misingi ya amani. Huyu mbwa mwitu anapokuwa huru, huvuruga kila kitu – hata mahusiano ya kijamii ambayo yamejengwa kwa miaka mingi.
Lakini hata baada ya kumfukuza mbwa mwitu, bado tunabaki na jukumu la kumdhibiti mwanambuzi. Mbuzi hapa ni lugha ya picha, ikituakisi sisi wananchi. Ni tabia zetu za kukimbilia upande mmoja bila kuchambua ukweli. Ni kupokea na kusambaza taarifa zisizo sahihi. Ni kushabikia siasa kwa jazba badala ya hoja. Tusipojizuia, tutabaki kuwa rahisi kuchochewa na kurejea katika mzunguko ule ule wa migogoro.
Katika kipindi hiki nyeti, nafasi ya viongozi wa dini ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Wanapaswa kuwa daraja la kuunganisha, si ukuta wa kutugawa.
Kauli zao zisiwe za upande mmoja, bali za haki na maridhiano. Vivyo hivyo, vyama vya upinzani vina wajibu wa kusimamia haki kwa njia za amani na kisheria, huku vikiepuka kuchochea hali inayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
Kwa upande wa serikali, ni lazima ionyeshe utayari wa kusikiliza na kujenga mazingira ya mazungumzo ya wazi. Nguvu peke yake haiwezi kujenga imani ya wananchi. Imani hujengwa kwa uwazi, haki na ushirikishwaji. Bila hivyo, hata juhudi za nje, zikiwamo za Chakwera, zitatoa furaha ya muda mfupi bila kuleta mabadiliko ya kudumu.
Sitanii, nafahamu fikira za kila upande kwa Watanzania wenzetu. Katika hili nasema, hata wapinzani waje mezani. Waitangulize Tanzania kwanza. Tusitarajie kuwa Mzungu ana nia ya kuijenga nchi yetu. Tufute lugha za matusi, dharau na kejeli katika upinzani kwa upinzani na upinzani na chama tawala. Kwa sasa kama nchi tumechagua tusi lisilo na mashiko.
Wadogo kwa wakubwa tusi kubwa au lugha tunayoiona ni fasheni, ni kutamka neno uchawa. Wapinzani kila wanayemwona au kudhani anaiunga mkono serikali, wanasema ni chawa huyo.
Sasa hata anayeunga mkono upinzani, unaambiwa ni chawa wa upinzani. Hii inatupa shida. Hivi neno chawa ni ajenda, ni sera? Lina uwezo wa kubadili maisha yetu yakawa mazuri. Binafsi nadhani mkakati huu wa neno chawa umefeli. Tutafute mbadala.
Sitanii, ukiniuliza mimi natamani kuona taifa linaloheshimiana. Natamani kuona taifa linalomheshimu Rais Samia Suluhu Hassan na kutambua mambo makubwa aliyoyafanya kwa nchi hii. Siwezi kuyarejea yote, maana ni mengi, ila angalau nitaje moja tu. Kila Januari ilikuwa tunakamatana kujenga madarasa na kutengeneza madawati, ila tangu ameingia madarakani Rais Samia hili limekwisha.
Upinzani nao tusiwachukulie poa. Nchi hii isingekuwa na upinzani, nakuhakikishia tungekuwa tunaitwa, tunachapwa viboko na kuambiwa tukalale saa 12 jioni. Si mnawakumbuka wakuu wa wilaya waliokuwa wanatesa watu na kusema ‘wanawaondoa wenge?’ Si tunakumbuka msamiati wa ‘watu wasiojulikana’ ulivyoshika kasi? Na kama si upinzani, watu wangeendelea kupotea! Namshukuru Rais Samia amedhibiti watu kupotea kiholela kwa sasa.
Sitanii, narudia, sitanii. Kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, bila kujali aina ya ushahidi uliopo, mimi, Deodatus Balile, siamini katika kufunguliana kesi. Iwe ni viongozi wa kisiasa au wa kijamii. Natamani na naomba kimyakimya na hadharani kuwa kesi wanazofunguliwa baadhi ya wanasiasa kama hii ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, sioni kama zina afya kwa jamii yetu.
Naomba niazime maneno ya Wazungu, japo siwapendi. “Apart from justification of law, there is amendment of law in order the law to act in accordance.” Katika fasiri isiyo rasmi, maneno haya yanamaanisha: “Mbali na kuhalalisha sheria, kuna marekebisho ya sheria, kuruhusu sheria kufanya kazi kulingana na mazingira.” Ndiyo maana jana, leo na kesho nasema, Tundu Lissu aachiwe.
Inawezekana Lissu alihemka, akatamka aliyoyatamka, ila umoja wetu ni zaidi ya maneno ya Lissu. Nashawishika tuwe na siku ya amani ya kitaifa. Siku hii tuwatoe hata mahabusu na wafungwa magerezani, tuzungumze katika mjadala wa wazi. Hapa ndipo namkumbuka Mzee (hayati) Kingunge Ngombare – Mwiru. Siku moja wakati ninamhoji alisema: “Ukweli ni kama mkuki, haupigwi konzi.” Sijui umenielewa?
Sitanii, nasema turejeshe umoja wa kitaifa. Lissu aachiwe, ila naye akiwa uraiani baada ya kuachiwa, apate marafiki wa kweli wa kumweleza kuwa hauwezi kusonga ugali kwa kiganja cha mkono, utaungua.
Wawe wazi kwake, wamweleze kuwa baadhi ya lugha zake hazina afya kwa ustawi wa jamii yetu. Lissu auganishe Watanzania kujikomboa kiuchumi.
Aambiwe kuwa mkoloni alikwishaondoka. Ajulishwe kuwa lugha za “Ma-CCM, Mwanamke, Mzanzibari, Mama Abdul… si sera itakayoleta ugali mezani. Atwambie kama anautaka urais, akichaguliwa sisi kama Tanzania watu wake ni lini watakuwa na uhuru wa kiuchumi?
Sayansi ya kurusha satellite itakuwa lini? Elimu yetu, SGR, afya, maji, umeme, huduma za kijamii, elimu… zitaimarika kwa kiasi gani? Hivi kutwambia ma-CCM itatutoa katika umaskini? Hapana, ila aachiwe tumweleze akiwa huru. DPP analiweza hili.
Ni muhimu pia kutambua kuwa umoja wa kitaifa hauji kwa kaulimbiu bali kwa vitendo. Tunahitaji kurejesha maadili ya kuheshimiana, kusikilizana na kukubali tofauti zetu kama sehemu ya nguvu ya taifa, si udhaifu wake. Hii ndiyo njia pekee ya kujenga mshikamano wa kweli.
Mwisho, tunapaswa kujiuliza: tunataka Tanzania ya namna gani? Je, ni taifa la migogoro isiyokwisha, au taifa la amani na maendeleo? Jibu limo mikononi mwetu.
Tukianza kwa kumfukuza mbwa mwitu wa vurugu na chuki, kisha tukajizuia sisi wenyewe tusichezee katika vichaka vya mgawanyiko, tutakuwa tumeweka msingi imara wa mustakabali bora.
Hapo ndipo tutakapoweza kusonga mbele kama taifa moja – lenye umoja, amani na mshikamano kwa maendeleo ya wote. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

