Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAZIRI wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kwa mwaka 2026 kitafanyika kitaifa katika Viwanja vya Dole, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho hayo, Waziri Shariff aliwataka wananchi, wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika hafla hiyo.
Aidha, aliwasisitiza wananchi na wafanyakazi kufika katika viwanja hivyo kuanzia saa 12:00 asubuhi ili kuhakikisha shughuli zinaanza kwa wakati, huku wizara, mashirika ya umma, taasisi binafsi na asasi zisizo za kiserikali zikihimizwa kuratibu usafiri kwa watumishi wao.
Alisema Serikali pia imeimarisha uratibu wa usafiri wa umma ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi katika viwanja hivyo na kushiriki kikamilifu katika tukio hilo muhimu la kitaifa.
“Niwaombe wananchi wote wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho haya, kwani Mei Mosi si siku ya wafanyakazi pekee bali ni siku ya kutafakari mchango wa kazi katika ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla,” alisema Waziri Shariff.
Shariff alifafanua kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatahusisha maandamano ya wafanyakazi, maonyesho ya magari ya kazi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, pamoja na salamu kutoka kwa viongozi wa kitaifa.
Aliongeza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, ambaye atahutubia katika kilele cha maadhimisho hayo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maadhimisho hayo yana lengo la kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika ukuaji wa uchumi wa taifa, kutathmini hali ya kazi ikiwemo maslahi, usalama na afya mahali pa kazi, pamoja na kuimarisha mshikamano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi.
Mapema alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi inaendelea kujitolea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kwa kuwa wao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
“Serikali inaendelea kutambua kuwa mazingira bora ya kazi ni chachu ya tija na maendeleo ya taifa, hivyo wafanyakazi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, uadilifu na uzalendo mkubwa,” alisema Waziri Shariff.
Mei Mosi ni kumbukumbu ya mapambano ya kihistoria ya wafanyakazi yaliyoanza mwaka 1886 huko Chicago, Marekani, ambapo wafanyakazi walidai haki zao za msingi ikiwemo mazingira bora ya kazi na muda wa kazi unaozingatia utu wa binadamu.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Upatikanaji wa haki na mazingira bora kazini ni msingi wa uwajibikaji, nidhamu na maadili ya wafanyakazi,” kauli inayolenga kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwiano kati ya haki za mfanyakazi na mazingira bora ya kazi ili kuongeza uwajibikaji, tija na maendeleo ya taifa.



