Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
WATU wawili wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa kufuatia mgogoro wa ardhi uliotokea katika eneo la Vikawe (Lupaso), Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza Mei 6, 2026, ofisini kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge amekiri kutokea tukio hilo la uvunjifu wa amani .
Amesema watu wasiojulikana walifika katika eneo hilo wakidaiwa kuwa na lengo la kuwaondoa wakazi wanaodaiwa kuvamia ardhi inayomilikiwa kihalali, hali iliyosababisha vifo vya watu wawili .
Kunenge alieleza kuwa majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo, mmiliki halali wa eneo pamoja na waliowatuma watu hao kwenda kuwaondoa wakazi.
Vilevile, amewataka wananchi kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi na uvamizi wa maeneo yasiyo yao.
“Wamiliki wa ardhi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria wanapokumbana na migogoro, ikiwemo kufikisha suala hilo katika mabaraza ya ardhi au mahakamani.
Pia,wamiliki endapo kuna amri ya mahakama ya kubomoa nyumba, washirikishe vyombo vya dola badala ya kuchukua hatua binafsi,” amesisitiza Kunenge.
Kwa upande wake, mkazi wa Chato, Vikawe, Kidawa Hamidu,
aliiomba Serikali ya Mkoa pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo ili haki ipatikane kwa pande zote.
Naye Mwenyekiti wa Vikawe Shule, Shaban Shaban, alisema mgogoro huo ulikuwepo muda mrefu na tayari vikao mbalimbali vilishafanyika kutafuta suluhu, lakini bado haijafahamika nani aliwatuma watu hao kwenda kuwaondoa wananchi.
“Coaster zilikuwa kama tano, wakiwemo watu zaidi ya 200 wakidai wametumwa kwenda kubomoa nyumba za watu waliovamia eneo hilo”
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Siaely Moshi, alithibitisha kupokea majeruhi hao sanjali na vifo vya watu wawili wanaume, akieleza kuwa majeruhi kumi wanaendelea kupatiwa matibabu na wengine wanaendelea vizuri.







