Na Mwandishi Wetu, Simanjiro

WEZI wawili wamehukumiwa na mahakama ya mwanzo Shambarai wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja kwa kosa la wizi wa ng’ombe wa thamani ya Sh2.5 milioni

Mshtakiwa wa kwanza Lazaro Miaroni mkazi wa kijiji cha Terrat wilayani Simanjiro na mshtakiwa wa pili Kutiti Mosori mkazi wa kijiji cha Komolo wilayani Simanjiro wamehukumiwa na hakimu mkazi wa mahakama ya mwanzo Shambarai, Aneth Mshendwa.

Watu hao wawili katika kesi hiyo namba 74 ya mwaka 2026 wamehukumiwa Mei 5, 2026 kwa kosa la wizi wa ng’ombe wa thamani ya Sh2.5 milioni mali ya Lenana Soipey mkazi wa kijiji cha Naisinyai wilayani Simanjiro.

Hakimu Mshendwa akisoma hukumu hiyo ameeleza kuwa washtakiwa hao waliiba ng’ombe mmoja katika kijiji cha Kitiangare wilayani Simanjiro mali ya Lenana Soipey mkazi wa kijiji cha Naisinyai.

Ameeleza kwamba washtakiwa hao wamefanya kosa la wizi wa ng’ombe katika shtaka la wizi wa mifugo chini ya kifungu cha 268 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2023.

Amesema kwa mujibu wa shahidi wa pili Oloimundi Nasambeni, mshtakiwa wa kwanza alikuwa amemshika kwa kamba ng’ombe huyo na wa pili alikuwa anamzuia wakati wakimswaga ng’ombe huyo.

Katika utetetzi wao washtakiwa hao wamedai kuwa walikabidhiwa ng’ombe huyo na mtu asiyejulikana wamuangalie kwa muda mfupi na mtu huyo ila hakurudi.

Shahidi wa kwanza wa kesi hiyo Lenana Soipey alimtambua ng’ombe wake kwa chapa ya moto iliyopo usoni mpaka mdomoni na nyuma ya mguu wa nyuma kwa juu tag ya njano ‘Lemala’ na rangi yake nyekundu.

Mmiliki wa ng’ombe huyo aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washttakiwa hao sababu ya vitendi kama hivyo vinakatisha tamaa katika ufugaji.

Lenana ameeleza mahakama hiyo kwamba ng’ombe kama huyu kumtunza hadi anakuwa na thamani inatumika gharama nyingi kumlisha kumtibu na kumwangalia kwa ujumla,

Amesema wezi hao wanafika kirahisi tuu na kumchukua ng’ombe huyo hivyo anaomba wapewe adhabu kali ili vitendo kama hivyo visijirudie tena.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza Miaroni, aliomba mahakama impunguzie adhabu na mshtakiwa wa pili Mosori, aliomba apunguziwe adhabu kwani anaomba msamaha kwa kufanya makosa.

Hakimu Mshendwa ameeleza kuwa japokuwa washtakiwa hao hawana rekodi ya makosa ya zamani wanapewa adhabu ya kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitano kila mmoja na haki ya rufaa imeelezwa ndani ya siku 30.