WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Mei 17, 2026 ameshiriki katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Kanda ya Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete, iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwigulu alimpongeza Nathan kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia pamoja na kuunga mkono juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.

Amesema kuwa imeshuhudiwa ongezeko kubwa na la kihistoria la ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia, ambapo takribani dola za Marekani bilioni 4.27 zilipatikana kupitia miradi na programu mbalimbali.

“Niruhusuni kwa mara nyingine kutoa shukrani zangu za dhati kwa Nathan kwa huduma yake ya kujitolea na mchango wake mkubwa katika safari ya maendeleo ya Tanzania, na kumtakia mafanikio mema katika majukumu yake mapya,” amesema Dkt. Mwigulu.

Aliongeza kuwa mchango wa Nathan katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia utaendelea kukumbukwa na kuthaminiwa.

“Mchango wako katika safari ya maendeleo ya Tanzania pamoja na kuimarisha ushirikiano wetu na Benki ya Dunia utaendelea kukumbukwa na kuthaminiwa daima. Nakushukuru sana,” amesema.

Kwa upande wake, Nathan Belete amesema anajivunia kazi iliyofanyika nchini Tanzania katika kipindi chake cha utumishi na kueleza kuwa ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa maendeleo ya nchi.

“Ninajivunia kazi ambayo tumeifanya nchini Tanzania. Ninajivunia mustakabali wa programu yetu hapa nchini. Ninaamini kuna fursa kubwa na za kipekee sana,” amesema Nathan.

Aidha, Amempongeza Dkt. Mwigulu kwa nia yake ya dhati ya kuiona Tanzania ikipiga hatua za kimaendeleo kutokana na jitihada zake kubwa za kufuatilia fedha za bajeti kutoka kwa washirika wa maendeleo.

“Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati huo, ambaye sasa ni Waziri Mkuu, alisema, tunahitaji kusukuma mageuzi. Ili nchi hii ikue na kubadilika, lazima tusukume mageuzi. Lakini huwezi kunipa fedha za kiwango cha kununua chapati ili kufanya mageuzi makubwa, na kwasasa fedha za bajeti kutoka benki ya dunia imekua kutoka dola za marekani milioni 250 hadi Dola Milioni 750″

Aidha, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya maendeleo ikilinganishwa na mataifa mengi barani Afrika kutokana na rasilimali na fursa zilizopo.

“Kama Mwafrika, huenda sipaswi kusema kwamba Tanzania ina uwezo mkubwa zaidi kuliko nchi nyingine, hata kuliko nchi yangu mwenyewe. Lakini kwa kweli naamini kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa zaidi kuliko nchi nyingi nyingine,” amesema.

Naye, Naibu Wazara wa Fedha Mhandisi Mshamu Ali Munde, amemshukuru Nathan kwa utumishi wake uliotukuka na mchango wake mkubwa katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Tanzania.

Kadhalika, amemuhakikishia Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia ajaye kuwa Wizara ya Fedha itafanya kazi kwa karibu naye katika kuendeleza vipaumbele vya maendeleo nchini hasa katika kipindi ambacho Tanzania inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050

Kwa Upande wake Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega amemshukuru Nathan kwa kusaidia utekekezaji wa miradi mbalimbali katika ya ujenzi nchini.

“Nathan hukuwa tu mwakilishi wa Benki ya Dunia, bali rafiki wa kweli wa matarajio yetu ya maendeleo. utaalam wako ulithaminiwa na imani yako katika maendeleo ya Tanzania iligusa mioyo ya wengi, Tanzania itaendelea itakukumbuka”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo amesema Nathan ameacha alama kubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini kupitia programu mbalimbali zilizofadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Tunatoa pongezi na shukrani zetu za dhati kwako, ndugu yetu Nathan, kwa huduma yako ya kujitolea kwa nchi yetu na hasa kwa sekta yetu. Uongozi wako, kujitolea kwako na ushirikiano wako umechangia kwa kiasi kikubwa safari ya maendeleo ya elimu nchini Tanzania, hususan katika mageuzi na maboresho yanayoendelea,” amesema Prof. Nombo.

Ameeleza kuwa kupitia programu ya SEQUIP, zaidi ya wasichana 10,000 waliokuwa katika hatari ya kukosa elimu wamewezeshwa kuendelea na masomo yao na kutimiza ndoto zao za kielimu.

“Kupitia mwongozo wako, ushirikiano kati ya nchi yetu na Benki ya Dunia umewezesha kufikisha matokeo yenye maana katika sekta ya elimu kwa mamilioni ya watoto wa Kitanzania,” ameongeza.

Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Bi. Sauda Msemo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia umekuwa na mchango mkubwa katika mageuzi ya sekta ya fedha nchini.

Amesema ushirikiano huo umechangia kuimarisha uwezo wa taasisi za kifedha, kukuza ujumuishwaji wa kifedha pamoja na kuongeza uimara na ufanisi wa mfumo wa fedha nchini.