Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), mwaka huu wadau wa biashara, wawekezaji, wabunifu na wananchi wanatarajiwa kushuhudia tukio la kipekee la kihistoria litakalojulikana kama “Sabasaba Golden Night”, Usiku wa Tuzo utakaofanyika tarehe 6 Julai 2026, usiku huu maalum wa dhahabu unalenga kusherehekea mafanikio, ubunifu na mchango wa maonesho hayo katika kukuza biashara na uchumi wa Tanzania kwa zaidi ya nusu karne.
Aidha,Uzinduzi wa Sabasaba Golden Night umebeba taswira mpya ya Maonesho ya Sabasaba ya mwaka 2026, ukiahidi burudani ya kiwango cha juu, mwangaza wa kipekee, maonesho ya kisasa, kutambua wadau waliotoa mchango mkubwa katika safari ya miaka 50 pamoja na kuunganisha sekta za biashara, uwekezaji na ubunifu chini ya jukwaa moja. Tukio hilo linatarajiwa kuwa moja ya vivutio vikubwa ndani ya Maonesho ya 50 ya Jubilei ya Dhahabu, yakiyotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, 2026.
Akizungumza Mgeni Rasmi Mhe. Dennis Londo amesema Tuzo hizo zitakazotolewa Mwaka huu zinalenga kuonesha ni kwa namna gani Sekta ya Biashara imekua kupitia maonesho ya Biashara ya Sabasaba na namna ambavyo Maonesho haya yamekuza maelfu ya wafanyabiashara amba sasa ni wakubwa.
Aidha Dkt.Latifa Mohammed Khamis Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo ya Biashara Tanzania ameeleza kuwa “Usiku wa Dhahabu” si burudani pekee, bali ni ishara ya heshima kwa safari ya mafanikio ya Sabasaba tangu kuanzishwa kwake, sambamba na kufungua ukurasa mpya wa fursa za biashara, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa. Wageni watakaohudhuria watapata nafasi ya kushuhudia historia ikikutana na ubunifu wa kizazi cha sasa katika mazingira yatakayobeba hadhi ya Jubilei ya Dhahabu. “Sabasaba 2026 KUBWA KULIKO











