Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam
CRDB Bank imeingia makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu na Bongo Star Search (BSS) kwa lengo la kuibua, kuendeleza na kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji mbalimbali nchini, kuanzia mwaka 2026 hadi 2028.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Mei 28, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo benki hiyo imeahidi kushirikiana na BSS katika kusaidia vijana wenye vipaji, sambamba na kuwapatia elimu ya fedha ili waweze kusimamia mafanikio yao kiuchumi baada ya kupata fursa kupitia vipaji vyao.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa CRDB, Steven Adili, alisema vijana ni nguvu ya uchumi wa sasa na wa baadaye, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwawekeza kwa kuwapa nafasi za kukuza vipaji pamoja na elimu ya kifedha.
Alisema katika kipindi hiki cha ukuaji wa teknolojia na mitandao ya kijamii, vijana wengi wanapata mafanikio kupitia ubunifu na vipaji vyao, jambo linalowafanya kuhitaji mwongozo wa kifedha ili mafanikio hayo yawe endelevu.
“CRDB Benki inawaona vijana kama kundi muhimu la uchumi wa leo na uchumi wa kesho. Ushirikiano wetu na Bongo Star Search unatokana na mchango wao mkubwa wa kuibua vipaji na kusukuma mbele ubunifu wa vijana wengi nchini,” alisema Adili
Aidha, Adili alisema benki hiyo itatoa kiasi cha shilingi milioni 260 katika kipindi cha miaka mitatu ya ushirikiano huo ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za BSS na kuwafikia vijana wengi zaidi wenye vipaji lakini wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa Bongo Star Search, Ritha Paulsen, aliishukuru CRDB kwa kuendelea kuiamini na kuunga mkono programu hiyo kwa misimu ya mwaka 2026, 2027 na 2028.
Ritha alisema ushirikiano huo utaongeza nguvu katika juhudi za kuibua vipaji vya vijana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uimbaji, utengenezaji wa maudhui ya burudani, ubunifu wa kidijitali na sekta nyingine za sanaa na ubunifu.
Alisema kupitia motisha hiyo, BSS itaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia vijana wenye vipaji na kuwapa nafasi ya kuonekana, kujifunza na kufikia ndoto zao.






