Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Benki ya Stanbic Tanzania imekuwa benki ya kwanza nchini kuzindua huduma ya Malipo ya Moja kwa Moja kwa Yuan ya China, inayowawezesha wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara na China kulipa na kupokea malipo kwa Yuan moja kwa moja bila kulazimika kupitia Dola ya Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Stanbic Tanzania, huduma hiyo inawahudumia waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na China, huku ikiwawezesha wafanyabiashara kupunguza gharama na muda unaotokana na ubadilishaji wa fedha.

Uzinduzi huo umefanyika Dar es Salaam Jumatano, Agosti 12, 2026, wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na China, ambayo imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Tanzania kwa miaka 10 mfululizo.

Stanbic imeeleza kuwa thamani ya biashara kati ya Tanzania na China imefikia karibu Dola za Marekani bilioni 9 katika miaka ya hivi karibuni, huku mfumo wa sasa wa kufanya miamala kupitia Dola ya Marekani ukiongeza gharama na muda wa baadhi ya miamala.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bwana Manzi Rwegasira, amesema huduma hiyo inalenga kurahisisha biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na China na kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

“China ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Tanzania, na imeshikilia nafasi hiyo kwa muongo mmoja. Huduma ya Malipo ya Moja kwa Moja kwa Yuan ya China inawapa wafanyabiashara wa Tanzania njia rahisi na ya moja kwa moja zaidi ya kufanya biashara na China,” amesema Rwegasira.

Amesema huduma hiyo inaenda sambamba na zana nyingine za kifedha zinazotolewa na Stanbic, ikiwemo ubadilishaji wa fedha za kigeni papo hapo, mikataba ya siku zijazo (forward contracts) na chaguo za kifedha (options), zinazolenga kuwasaidia wafanyabiashara kudhibiti hatari za mabadiliko ya thamani ya fedha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo, amesema matumizi ya RMB yanaendana na lengo la kupunguza vikwazo visivyo vya lazima kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na masoko muhimu ya kimataifa.

“Lengo letu si kuhamasisha matumizi ya sarafu fulani, bali kuhakikisha wafanyabiashara wanapata njia za malipo zilizo bora, salama na za kuaminika zinazowawezesha kutumia fursa zilizopo,” amesema Msemo.

Ameongeza kuwa BoT itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayoruhusu ubunifu wa kifedha huku ikihakikisha uthabiti, uadilifu na uimara wa mfumo wa kifedha nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema uzinduzi wa huduma hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya fedha na biashara, kupunguza vikwazo katika miamala na kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki kwa ufanisi zaidi katika masoko ya kimataifa, hususan China.

Amesema Tanzania inapaswa kuimarisha uhusiano kati ya fedha, uzalishaji na masoko ili kujenga mfumo jumuishi unaounga mkono Dira ya Tanzania 2050, kuongeza mauzo ya nje, kuunda ajira na kuwawezesha wafanyabiashara kushindana katika masoko ya kimataifa.

Mkuu wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa Stanbic Tanzania, Bi. Ester Manase, amesema huduma hiyo itawasaidia waagizaji na wasafirishaji wakubwa kusimamia hatari za mabadiliko ya thamani ya fedha na kuachia mtaji wa uendeshaji ambao ungeweza kutumika katika gharama za ubadilishaji wa fedha.

Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME), Stanbic imeeleza kuwa waagizaji wanaolipa moja kwa moja kwa Yuan kwa wauzaji wa China wanaweza kupunguza gharama za ubadilishaji wa fedha na kupata nafasi zaidi ya kujadiliana bei na masharti ya malipo.

Kwa wasafirishaji wa Tanzania kwenda China, huduma hiyo pia inalenga kuwezesha malipo ya moja kwa moja na ya haraka zaidi kwa bidhaa zinazouzwa katika soko hilo.

Stanbic imeeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 za Afrika zilizoainishwa kuwa nchi maskini zaidi duniani (LDC) zilizopewa unafuu wa ushuru wa asilimia 100 na China tangu Desemba 2024, jambo linalotoa fursa kwa wasafirishaji wa bidhaa za kilimo kama parachichi, soya na ufuta.

Mkuu wa Huduma za Kibiashara kwa Wateja wa Kati katika Stanbic Tanzania, Fredrick Max, amesema malipo ya moja kwa moja kwa Yuan yanaweza kupunguza gharama za ubadilishaji fedha na kuwawezesha wafanyabiashara kujadiliana zaidi kuhusu bei na masharti ya malipo.

Amesema kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaouza bidhaa China, malipo ya moja kwa moja yanaweza kuwawezesha kulipwa kwa haraka na kwa uhakika zaidi.

Huduma hiyo inapatikana kwa wateja wa makampuni makubwa, wafanyabiashara wa kati na wadogo (SME), pamoja na wateja binafsi, kwa kuzingatia miongozo ya kisheria ya Benki Kuu ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, huduma ya Malipo ya Moja kwa Moja kwa Yuan ya China imewezeshwa na uwezo wa Standard Bank Group, kampuni mama ya Stanbic Tanzania, ambayo kwa kushirikiana na Benki ya Viwanda na Biashara ya China (ICBC), imeidhinishwa na Benki Kuu ya China (People’s Bank of China) kufanya shughuli za usafirishaji wa fedha za Yuan barani Afrika.

Standard Bank imeidhinishwa mwaka 2026 na sasa inafanya kazi kama Benki Msafirishaji wa Yuan ya China barani Afrika (Renminbi Clearing Bank of Africa), hatua inayowezesha huduma hiyo kutolewa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Stanbic Tanzania imewahimiza wafanyabiashara wanaofanya biashara na China, wakiwemo wanaoagiza mitambo na bidhaa au kusafirisha mazao ya kilimo na bidhaa zilizotengenezwa, kuwasiliana na benki hiyo ili kufahamu namna huduma hiyo inavyoweza kupunguza gharama na kurahisisha miamala yao ya kibiashara.

 Kushoto, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo; Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira; na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, wakiwa pamoja na wadau wengine wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo wa CIPS na huduma ya malipo ya moja kwa moja kwa Yuan ya China (RMB), jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo unaifanya Stanbic Bank Tanzania kuwa benki ya kwanza nchini kuwezesha wafanyabiashara wanaofanya biashara na China kutuma na kupokea malipo moja kwa moja kwa Yuan, bila kulazimika kubadilisha fedha kupitia Dola ya Marekani.