ARUSHA, Agosti 28, 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Fedha na Kilimo kuandaa mpango wa mafunzo kwa Vitendo ambao utaanza kuchukua walau vijana 10,000 kupata uzoefu katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Sekta binafsi ili kuandaa vijana watakaokuwa na uzoefu wa kujiajiri na kuajiriwa kama sehemu muhimu ya kutekeleza nguzo ya pili ya Dira ya Taifa 2050 na kusaidia maendeleo ya Nchi.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma kubadili namna taasisi hizo zinavyofanya kazi na kuwa injini ya mageuzi ya uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akielekeza kuanzishwa kwa mkakati huo utakaowapatia angalau wahitimu 10,000 nafasi za mafunzo kwa vitendo na kuwapatia fedha za kujikimu katika mashirika ya umma na wengine wasiopungua 20,000 katika sekta binafsi.

” Kila mwaka kwa takribani vijana 62,570 wanahitimu elimu ya juu na hii ni takwimu ya mwaka Jana 2025 toka TCU, idadi hiyo haihusishi wale wanaomaliza VETA na Vyuo vya Kati. Ukiangalia TAESA takwimu zao zinaonesha vijana 3,200 pekee walikuwa wamepitia programu za mafunzo internship, idadi hii ni ndogo sana kwa kulinganishwa na wahitimu 62,570 kutoka vyuo mbalimbali nchini. Mlitazame hili kama uwekezaji wa kimkakati katika nguvu kazi ya Taifa kwa kubana matumizi ya kawaida, na hapa mtakuwa mmetekeza kwa Vitendo nguzo ya pili ya Dira 2050″ alisisitiza

Mhe. Ndejembi, amesema dhamana ya Watendaji, Wakuu wa Mashirika na Wenyeviti wa Bodi ni kubwa, na hivyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na umakini mkubwa na kwa wakati sahihi katika kujenga uchumi, kuibua fursa mpya na kuinua maisha ya watanzania.

“Mashirika ya Umma yana nafasi ya kipekee katika kufikia malengo ya Dira 2050 kutokana na dhamana yake ya kusimamia mali za umma, kuendesha miundombinu ya kimkakati, kutoa huduma muhimu za nishati, usafirishaji, mawasiliano, fedha, afya, maji, na nyingine zinazobeba uchumi wetu. Kutokana na hilo, lazima tuyaangalie mashirika hayo kama injini ya mageuzi makubwa ya kiuchumi tunayoyalenga katika Dira 2050.” alisisitiza Ndejembi.

Sambamba na ajira na ujuzi kwa vijana, Makamu wa Rais amezitaka Taasisi na Mashirika ya Umma ukiangalia namna ya kupunguza matumizi yasiyo na tija na utegemezi kwa Serikali, huku zikibuni vyanzo endelevu vya mapato na kuhakikisha kila shilingi ya umma inaleta thamani inayostahili.

Ili kuhakikisha maelekezo hayo yanatafsiriwa kuwa matokeo, Ndejembi ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha mfumo wa tathmini ya utendaji wa mashirika ya umma, na kutambua kwenye tuzo za mwaka ujao Taasisi zitakazotekeleza agizo la kuchukua vijana na kuwapa mafunzo.

Amehitimisha kwa kuzitaka Taasisi na Mashirika kujiandaa mapema kukabiliana na athari za mvua za El Niño ili kulinda miundombinu na uwekezaji wa umma na kuhakikisha huduma muhimu kwa wananchi haziathiriki.

Kikao hicho cha C-CEOs Forum 2026 kimewakutanisha jijini Arusha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, pamoja na Mawaziri, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Makatibu Wakuu na viongozi wengine wa Serikali.

Kikao hicho cha siku tatu kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kutoa mwelekeo wa kimkakati kuhusu mustakabali wa Mashirika ya Umma, kutathmini yalipotoka na kujadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuongeza mchango wake katika uchumi na maendeleo ya Taifa, hususan wakati Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.