Mwenyekiti wa Makampuni ya Mati Group, David Mulokozi, ameshiriki kama Mgeni Rasmi katika Ibada ya Harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mt. Maria Mama wa Mungu Kibondo, lililopo Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mulokozi amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa na moyo wa kutoa, akieleza kuwa kutoa ni sehemu ya ibada na kwamba baraka nyingi za Mungu hujificha katika moyo wa ukarimu na kujitoa.
“Kuna baraka nyingi zimejificha katika kutoa, Mungu ameweka ahadi za moja kwa moja ikiwemo ulinzi wako binafsi, familia yako, na hata mali zako, kila tunachokifanya kinaambatana moja kwa moja na kutoa kwa moyo.” amesema Mulokozi.
Katika harambee hiyo, jumla ya Shilingi milioni 327,118,250 zimekusanywa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kanisa, ambapo Mulokozi amechangia Shilingi milioni 158, kiasi kilichokuwa sehemu kubwa ya mchango wote uliopatikana siku hiyo.
Kwa upande wake, Baba Askofu wa Jimbo la Kigoma, Joseph Romanus Mlola, amemshukuru David Mulokozi kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi wa harambee hiyo pamoja na mchango wake mkubwa uliochangia kufanikisha lengo la shughuli hiyo.
Askofu Mlola pia amempongeza Mulokozi kwa uwekezaji mkubwa anaouendelea kuufanya nchini kupitia Makampuni ya Mati Group, akisema uwekezaji huo unaendelea kutoa mchango muhimu katika kuzalisha ajira kwa Watanzania na kuongeza pato la taifa.
Mafanikio makubwa ya harambee hiyo, yanasaidia kuharakisha ujenzi wa kanisa hilo na kuimarisha huduma za kiroho kwa waumini wa Parokia ya Mt. Maria Mama wa Mungu Kibondo mkoani kigoma.

