āSerikali yapongezwa kwa kuimarisha sekta ya madini, wawekezaji waendelea kuonesha imani kubwa
šDAR ES SALAAM
Wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo kupitia uwazi, utekelezaji wa sheria na matumizi ya mifumo rasmi ya biashara, hatua ambazo zimeongeza imani ya wawekezaji, ufanisi wa biashara na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na mfanyabiashara mkubwa wa madini ya Tanzanite nchini, Taikoo Kulunju Oletipa, baada ya kutembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Taikoo amesema maboresho yanayotekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Madini yameendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuongeza tija katika shughuli za madini.
āSerikali kupitia Tume ya Madini imekuwa ikiwashirikisha na kuwasikiliza wadau wa sekta hii, jambo ambalo limewezesha kufanyika kwa maboresho yanayochochea ukuaji endelevu wa sekta ya madini nchini,ā amesema.
Aidha, amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha wadau na wananchi kufahamu kwa kina utajiri mkubwa wa rasilimali madini zilizopo nchini pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara.
Taikoo amesema licha ya uzoefu wake wa muda mrefu katika biashara ya madini ya Tanzanite na dhahabu, maonesho hayo yamemuwezesha kujionea aina nyingine za madini yenye thamani kubwa na fursa zake za kiuchumi.
āNimekuwa nikijihusisha na biashara ya Tanzanite na dhahabu kwa muda mrefu, lakini kupitia maonesho haya nimepata fursa ya kujionea madini mengine kama chuma kutoka Liganga na Lithium. Tanzania ina hazina kubwa ya rasilimali madini ambazo zinahitaji kuendelea kutangazwa na kuendelezwa kwa manufaa ya Watanzania,ā amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (CHAMATA), Mokia Ole Mrefu, amesema hatua za Serikali kufungua fursa mpya za uchimbaji wa madini ya vito mkoani Manyara zinaakisi dhamira ya kupanua wigo wa biashara ya madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Amesema eneo ambalo kwa muda mrefu lilifahamika zaidi kwa uzalishaji wa madini ya Tanzanite sasa linafungua milango ya uwekezaji katika madini mengine ya vito, hali inayoongeza ushindani na fursa za biashara.
āTanzania ina utajiri mkubwa wa madini na maonesho haya yametupa picha halisi ya wigo mpana wa fursa zilizopo katika sekta hii, kuanzia uchimbaji, biashara, uongezaji thamani hadi uwekezaji katika viwanda vinavyotegemea madini. Hii ni fursa muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa,ā amesema.










