Waiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu madini na fursa za uwekezaji

📍DAR ES SALAAM

Madini ya Tanzanite yameendelea kuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku mamia ya wananchi wakifurika katika Banda la Tume ya Madini kujionea kwa karibu jiwe hilo la thamani linalopatikana Tanzania pekee duniani pamoja na kupata elimu kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu ya “Fahari ya Tanzania” yalianza rasmi Juni 28, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13 2026, sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo makubwa ya biashara nchini.

Miongoni mwa wananchi waliotembelea banda hilo ni Nuru Maliki, ambaye amesema ameridhishwa na elimu na huduma alizopata pamoja na nafasi ya kujionea madini mbalimbali ambayo awali alikuwa akiyasikia kupitia historia na simulizi pekee.

“Nimepata huduma nzuri sana na fursa ya kujionea madini mbalimbali, hususan Tanzanite na madini mengine yanayopatikana hapa nchini. Kuna baadhi nilikuwa nikiyasikia tu katika historia, lakini leo nimeyaona kwa macho yangu,” amesema.

Kwa upande wake, Eveline Natai amesema maonesho hayo yameongeza uelewa wake kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini na kumhamasisha kuanza kupanga namna ya kushiriki katika shughuli za sekta hiyo.

“Nimefurahishwa kuona madini mbalimbali na kupata taarifa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo. Nitajipanga kuingia katika sekta hii. Serikali iendelee kutoa elimu kwa Watanzania ili watu wengi zaidi wajifunze na kunufaika na fursa zinazotokana na rasilimali za madini,” amesema.

Akitoa elimu kwa wananchi, Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Abbas Mruma, amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwaelimisha wananchi kuhusu rasilimali za madini, matumizi yake pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.

Naye Mjiolojia Mwandamizi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mirerani, Seleman Khamis, amesema thamani ya madini ya Tanzanite hupimwa kwa kuzingatia vigezo vinne muhimu ambavyo ni rangi, uzito, ubora na umbo.

Amefafanua kuwa rangi kuu za Tanzanite ni bluu na zambarau, huku akibainisha kuwa madini hayo yanapatikana Tanzania pekee katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, jambo linaloyafanya kuwa miongoni mwa madini ya vito yenye upekee na thamani kubwa zaidi katika soko la kimataifa.

Mvuto mkubwa wa Tanzanite katika maonesho hayo umeendelea kuthibitisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha madini ya vito duniani, huku wananchi wakizidi kuhamasika kufahamu zaidi kuhusu sekta ya madini na fursa zake za uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.

Wakati huohuo, viongozi mbalimbali wametembelea banda la Tume ya Madini, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse.

Viongozi hao wamepongeza kazi kubwa ya utoaji elimu na uhamasishaji kuhusu sekta ya madini inayotekelezwa na Tume ya Madini, wakieleza kuwa imechangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo na mchango wake kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.