✅️ Tanzania yaendelea kujijengea nafasi ya kipekee duniani kama kitovu cha tafiti za miamba ya shinikizo la juu na utalii wa kijiolojia.

✅️ Profesa Abdulkarim Mruma Ahusika na Kuendeleza Urithi wa Tafiti za Mautia Hill

📍Kongwa – Dodoma

Katika eneo la Mlima wa Mautia, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Tanzania kunapatikana moja ya hazina adimu zaidi za kijiolojia duniani, madini ya Yoderite. Madini haya yameifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama sehemu muhimu ya tafiti za jiolojia, huku yakifungua fursa mpya za utalii wa kijiolojia (geotourism), elimu na utafiti wa kisayansi.

Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza duniani mwaka 1959 katika Mlima wa Mautia, kupitia utafiti wa kihistoria ulioongozwa na mwanajiolojia Hatten Yoder Jr kutoka Marekani. Ugunduzi huo uliiweka Tanzania katika ramani ya dunia ya sayansi ya jiolojia na kuifanya Mautia Hill kuwa eneo lenye umuhimu wa kipekee wa kisayansi. Baadaye, aina hiyo ya madini iliripotiwa kugunduliwa tena nchini Zimbabwe mwaka 1998, jambo linalothibitisha kuwa Yoderite ni madini yanayopatikana katika maeneo machache sana duniani.

Kwa mujibu wa tafiti za jiolojia, Yoderite pamoja na miamba ya metamofia inayojulikana kama whiteschists iliundwa takribani miaka milioni 630 iliyopita, chini ya mazingira yenye shinikizo na joto kali sana ndani ya ganda la dunia. Wakati wa mabadiliko ya sahani za dunia (plate tectonics), miamba hiyo ilisafirishwa kutoka kina kinachokadiriwa kuzidi kilomita 30 hadi 35 chini ya uso wa dunia. Baadaye ilifika karibu na uso kupitia michakato ya kuinuka kwa miamba (tectonic uplift). Miamba hiyo imekuwa ushahidi muhimu unaowasaidia wanasayansi kuelewa jinsi sehemu za ndani kabisa za dunia zilivyobadilika katika historia yake ya mamilioni ya miaka.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo katika ziara maalumu, Meneja wa Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Solomon Maswi, alisema Yoderite si madini yanayolenga uchimbaji wa viwandani bali ni urithi wa kisayansi wenye thamani kubwa katika elimu, tafiti na utalii wa kijiolojia. Alisema upekee wa madini hayo unaifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kipekee duniani kama kitovu cha tafiti za miamba ya shinikizo la juu, huku Mlima wa Mautia ukiendelea kubeba historia muhimu ya mageuzi ya ndani ya dunia.

Kwa mujibu wa Maswi, Yoderite haitazamwi kama madini ya uchumi kwa sababu hupatikana kwa uchache sana duniani, haina akiba kubwa ya kibiashara wala matumizi ya moja kwa moja katika uzalishaji wa viwandani. Badala yake, thamani yake kubwa ipo katika mchango wake kwa maendeleo ya sayansi, elimu ya jiolojia na uhifadhi wa urithi wa asili. Kutokana na umuhimu huo, wataalamu wanashauri Yoderite ihifadhiwe kama “maabara ya asili” inayowawezesha wanafunzi, watafiti na wanasayansi kutoka duniani kote kujifunza historia ya mabadiliko ya ganda la dunia.

Mautia Hill: Kituo cha Tafiti za Kimataifa kwa Zaidi ya Miaka 60

Umuhimu wa Mlima wa Mautia katika tafiti za jiolojia umeendelea kuthibitishwa kwa zaidi ya nusu karne tangu ugunduzi wa Hatten Yoder Jr mwaka 1959. Eneo hilo limeendelea kuvutia wataalamu mashuhuri wa jiolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Miongoni mwao ni Profesa Abdulkarim Mruma, ambaye kati ya mwaka 1981 na 1983 alifanya utafiti katika Mlima wa Mautia akishirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Göttingen, Ujerumani. Katika kipindi hicho pia alifanya utafiti wake wa Shahada ya Uzamili wa Sayansi (MSc) chini ya usimamizi wa Profesa Helmut Behr, uliochangia kuongeza uelewa kuhusu miamba yenye shinikizo la juu na madini adimu ya eneo hilo. Kwa miongo kadhaa, watafiti wengine kutoka Göttingen na taasisi nyingine za kimataifa, akiwemo Dkt. Tillman Henrichs, wameendelea kufika Mautia kufanya tafiti mbalimbali, wakichangia kuifanya Kongwa catabolic katika duru za kimataifa za sayansi ya jiolojia.

Fursa ya Geotourism kwa Tanzania

Mbali na umuhimu wake wa kisayansi, Mlima Mautia una uwezo mkubwa wa kuwa kivutio cha utalii wa kijiolojia, ambapo wanafunzi, watafiti, wanajiolojia na watalii kutoka duniani kote wanaweza kutembelea eneo hilo kujifunza historia ya dunia kupitia miamba yake ya kipekee. Maendeleo ya geotourism yanaweza kuongeza thamani ya eneo hilo kupitia uanzishwaji wa vituo vya tafsiri ya jiolojia (Geological Interpretation Centres), njia maalumu za kutembelea miamba (geotrails), programu za elimu kwa wanafunzi na ushirikiano wa kimataifa katika tafiti za sayansi ya dunia.

Kwa kufanya hivyo, Kongwa inaweza kujijengea hadhi ya kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi ya geotourism barani Afrika, huku ikihifadhi urithi wake wa kipekee kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Mageuzi ya Kongwa yanaashiria dira mpya ya Tanzania katika usimamizi wa rasilimali za kijiolojia, kutoka mtazamo wa uchimbaji pekee kuelekea uhifadhi, elimu, tafiti na utalii wa kisayansi.