Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Katika hatua mpya ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kujenga taifa lenye afya, Serikali imezindua Mkakati wa Huduma Jumuishi za Usafi wa Mazingira, ukilenga kuimarisha usimamizi wa taka, majitaka na huduma za usafi nchini ili kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ustawi wa wananchi.

Uzinduzi wa mkakati huo umefanyika leo July 2,2026 Jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililowakutanisha viongozi wa Serikali, Bunge, taasisi za udhibiti pamoja na wadau wa sekta ya maji na mazingira, kwa lengo la kuweka msingi wa mageuzi ya usimamizi wa huduma za usafi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Paramagamba Kabudi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira kuwa moja ya ajenda kuu za maendeleo kutokana na mchango wake katika kulinda afya za wananchi, kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo endelevu.

Kabudi amesema Tanzania inalenga kujenga miji na vijiji vilivyo safi, salama na vinavyosimamiwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi wa mazingira, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yatawezekana kupitia mabadiliko ya tabia kwa wananchi sambamba na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya usafi.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha huduma jumuishi za usafi wa mazingira zinawafikia wananchi wote bila kujali wanaishi mijini au vijijini, hatua itakayopunguza athari za magonjwa yanayotokana na mazingira machafu na kuboresha ubora wa maisha.

“Tunajenga Taifa ambalo usafi wa mazingira ni sehemu ya maisha ya kila siku,hili haliwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa Serikali na wananchi,” amesema Kabudi.

Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiongoza ajenda ya nishati safi ya kupikia duniani, akisema matumizi ya nishati hiyo yanasaidia kupunguza ukataji wa miti, uchafuzi wa hewa na madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya nishati chafu.

Kabudi pia alionya kuhusu tabia ya kutupa taka kwenye mitaro ya maji ya mvua, akisema hali hiyo inachochea kuziba kwa mifumo ya maji, huongeza hatari ya mafuriko na kuharibu mazingira ya mijini.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika usafi wa mazingira ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya ya jamii, ukuaji wa uchumi na kuongeza uwezo wa miji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, amesema changamoto nyingi za mazingira zinazochangia magonjwa na vifo zinaweza kupunguzwa kwa kuimarisha elimu ya mazingira na usimamizi katika ngazi zote.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe, alisema bado kuna pengo kubwa katika usimamizi wa majitaka nchini, akibainisha kuwa mamlaka 24 pekee kati ya 84 ndizo zenye mipango ya kutibu majitaka na tope la kinyesi.

Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa utekelezaji wa Mkakati mpya wa Huduma Jumuishi za Usafi wa Mazingira ili kuhakikisha miji na makazi ya wananchi yanakuwa safi, salama na yenye mifumo endelevu ya usimamizi wa taka

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ongezeko la idadi ya watu jijini Dodoma linaongeza shinikizo kwenye huduma za usafi wa mazingira, hivyo kuna haja ya kupanga na kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kisasa ya usafi.

Kongamano hilo limeelezwa kufungua ukurasa mpya wa usimamizi wa mazingira nchini, ambapo Serikali, taasisi na wananchi wanatarajiwa kushirikiana katika utekelezaji wa Mkakati wa huduma Jumuishi za Usafi wa Mazingira ili kujenga Tanzania yenye mazingira safi, afya bora na maendeleo endelevu.