Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Maendeleo ya Vijana), Joel Nanauka, amewapongeza vijana wenye mahitaji maalumu wanaojishughulisha na fani mbalimbali, ikiwemo usanifu majengo na ushonaji, waliopo katika banda la VETA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo na kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na vijana hao,Julia 3,2026 Waziri Nanauka alisema Serikali inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ili isomane na kuwezesha vijana wote wanaojisajili kutambulika kwa urahisi na kunufaika na fursa zinazotolewa.
Kwa upande wake, kijana mwenye mahitaji maalumu, Francis Madanya, aliyebuni power bank yenye uwezo wa kuchaji simu kwa muda wa hadi saa tatu, alisema anaishukuru VETA kwa kumpatia ujuzi uliomwezesha kubuni bidhaa hiyo.
Alisema ujuzi alioupata utamwezesha kuzalisha bidhaa zaidi, kujiajiri na kuinua hali yake ya kiuchumi kupitia ubunifu.
Naye Joseph Mtei, kijana mwenye mahitaji maalumu aliyepata mafunzo ya usanifu majengo kwa kutumia kompyuta, alisema licha ya kutokuwa na mikono, hutumia miguu yake kuendesha kompyuta na kutengeneza ramani za majengo.
“Mimi sina mikono, natumia miguu yangu kutengeneza ramani za majengo. Nashukuru Mungu kwa fani niliyo nayo. Nikipata zabuni mbalimbali, nitajipatia kipato na kujikwamua kiuchumi,” amesema Joseph Mtei.
Vijana hao wameeleza kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na VETA yamekuwa chachu ya kuwawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi.



