Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeibuka mshindi wa kwanza katika tuzo za Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), baada ya kutambuliwa kwa kufanya vizuri kupitia bidhaa zake za kilimo na uvuvi.

Akizungumza Julai 3,2026 mara baada ya kupokea tuzo hiyo katika banda la JKT lililopo kwenye maonyesho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonyesho ya Sabasaba na Nanenane, Brigedia Jenerali Shija Lubi, alisema ushindi huo ni mwendelezo wa mafanikio ambayo JKT imekuwa ikiyapata kwa miaka kadhaa kutokana na ubora wa bidhaa zake zinazozalishwa kupitia viwanda na mashamba yake.

Alisema mwaka uliopita JKT ilishinda tuzo katika kundi la bidhaa za samani (furniture), huku mwaka huu ikiamua kushindana katika sekta ya kilimo na uvuvi na kufanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza.

“Mwaka jana tulimshukuru Mungu kwa kuibuka washindi katika bidhaa za samani. Mwaka huu tukaamua kushindana katika bidhaa za kilimo na uvuvi, na tumefanikiwa tena,” alisema Brigedia Jenerali Lubi.

Alieleza kuwa siri ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, ambaye amekuwa akisisitiza uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya ubora kupitia vikosi na Shirika la Uzalishaji Mali la JKT.

Brigedia Jenerali Lubi alisema JKT linaendelea kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo na utaalamu katika sekta za kilimo na uvuvi kwa wananchi wanaohitaji bure bila malipo

Aliongeza kuwa mbali na kilimo na uvuvi, JKT linaendelea kuimarisha shughuli za ufugaji kwa kutumia ranchi zake zilizopo Misenyi, Mafinga na Morogoro. Pia linaendelea na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kisasa cha kuchakata maziwa ya ng’ombe, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Alisisitiza kuwa JKT itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya uzalishaji ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.