Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarisha juhudi za kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini kwa kuwahamasisha wananchi waliojiajiri kujiunga na Hifadhi Skimu, huku ukiwahimiza waajiri wenye malimbikizo ya michango kunufaika na msamaha wa tozo uliotolewa na Mfuko. Wito huo umetolewa wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumza baada ya kutembelea banda la NSSF katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema ameridhishwa na mwitikio wa wananchi pamoja na huduma zinazotolewa na Mfuko, hususan elimu kuhusu hifadhi ya jamii, usajili wa wanachama wapya na huduma za kidijitali.
Bw. Mshomba alisema banda la NSSF limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu nafasi ya hifadhi ya jamii katika kuboresha ustawi wa maisha, kupunguza umaskini, kuimarisha nguvu kazi na kuongeza uzalishaji katika uchumi wa taifa.
Kupitia Hifadhi Skimu, alisema wananchi waliojiajiri wanaweza kujiunga na NSSF kwa hiari na kuchangia kwa viwango vinavyolingana na uwezo wao.
Alieleza kuwa kiwango cha chini ni shilingi 30,000 kwa mwezi kinachomwezesha mwanachama kupata huduma za matibabu, huku mchango wa shilingi 52,200 ukimpa mwanachama huduma za matibabu yeye mwenyewe, mwenza wake na watoto wasiozidi wanne.
Alifafanua kuwa wanachama wa skimu hiyo pia hunufaika na mafao ya uzazi, ulemavu, pensheni ya uzee na urithi, akibainisha kuwa mfumo huo unaruhusu michango kufanyika hata kila siku ilimradi ifikie kiwango cha mwezi.
Bw. Mshomba alisema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameongeza ushiriki wa wananchi waliojiajiri katika mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii.
Katika huduma za kidijitali, alisema NSSF imeboresha mifumo yake inayowezesha wanachama na waajiri kujihudumia popote kupitia NSSF Portal bila kufika ofisini, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Bw. Mshomba alisema NSSF imetoa msamaha wa tozo kwa waajiri wenye madeni ya michango kuanzia Juni hadi Desemba 2026, ili kuwapa fursa ya kulipa madeni ya msingi na kupunguza mzigo wa tozo.
Alisema waajiri watakaolipa madeni yao ya msingi kuanzia Juni hadi Agosti 31, 2026 watanufaika na msamaha wa asilimia 100 ya tozo, mradi waendelee kulipa michango ya sasa kwa wakati hadi Januari 2027. Wataakaoanza kulipa kati ya Septemba 1 na Oktoba 31 watanufaika na msamaha wa asilimia 75, huku watakaoanza kulipa kati ya Novemba 1 na Desemba 31 wakinufaika na msamaha wa asilimia 50.
Aliwataka waajiri kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uzalishaji badala ya kuelekeza rasilimali katika kulipa tozo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango kwa wakati ili kulinda haki za wafanyakazi.
Pia aliwahimiza waajiriwa kufuatilia michango yao na kutoa taarifa NSSF endapo michango yao haiwasilishwi kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia ukuaji wa Mfuko, Bw. Mshomba alisema thamani ya NSSF imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.8 mwezi Machi 2021 hadi shilingi trilioni 9.8 kufikia Juni 30, 2026 kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku hesabu ambazo bado hazijakaguliwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2026, zikionesha thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 11.6.
Alieleza kuwa ukuaji huo umetokana na ongezeko la michango, uwekezaji wenye tija pamoja na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wa uwekezaji, alisema NSSF imeanza kuwekeza nje ya nchi baada ya kupata kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikilenga masoko ya mitaji na miradi ya majengo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikiwemo ujenzi wa majengo ya biashara jijini Nairobi, Kenya, yatakayoongeza mapato na kuimarisha uwezo wa Mfuko.










