Na. Mwandishi Wetu
TUME ya Ushindani (FCC) imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wajasiriamali kutoka Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kuhusu namna ya kutambua bidhaa bandia, kulinda haki za walaji na biashara ili kuimarisha ushindani wa haki nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa FCC, Bi. Roberta Feruzi, amesema maonesho hayo yameiwezesha tume hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapa elimu kuhusu haki za walaji, ulinzi wa biashara pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na FCC.
“FCC inaendelea kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi, kusajili mikataba na kutoa huduma nyingine zinazolenga kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara.”amesema
Aidha FCC imewahimiza wananchi na wafanyabiashara kuendelea kutumia fursa ya maonesho hayo kupata elimu, kuripoti bidhaa bandia na ukiukwaji wa haki za biashara ili kujenga mazingira ya ushindani wa haki na kulinda maslahi ya walaji nchini.
Kwa upande wake Afisa Ushirikiano wa TWCC, Bw. Nelson Clevary, ameipongeza na kuishikuru FCC kwa mafunzo hayo, akisema yamewasaidia wajasiriamali kutambua bidhaa bandia, kulinda bidhaa zao na kuelewa umuhimu wa kusajili majina na nembo za biashara.
Amesema ushirikiano wa miaka mitatu kati ya TWCC na FCC umeongeza uelewa wa wafanyabiashara kuhusu athari za bidhaa bandia na umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika katika kukabiliana na vitendo vya udanganyifu wa kibiashara.
Naye mjasiriamali kutoka Mwanza, Praxeda Mgyabuso, amesema elimu inayotolewa na FCC imewasaidia wafanyabiashara na wananchi kutofautisha bidhaa halisi na bandia pamoja na kuelewa umuhimu wa kulinda utambulisho wa biashara zao.
Amesema awali wengi walikuwa wakinunua bidhaa kwa kuangalia bei pekee, lakini sasa wanafahamu athari za bidhaa bandia kwa afya, uchumi na biashara, pamoja na umuhimu wa kusajili alama na nembo za biashara.










