📌Waziri Ndejembi asema ni tukio la kihistoria litakaloshuhudiwa na watanzania pamoja na wageni
📌Asema mradi wa JNHPP ni matokeo ya uwekezaji wa sh.trilioni 7.4; Fedha za Watanzania
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, tarehe 22 Agosti 2026, katika eneo la mradi lililopo Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Amesema hayo tarehe 15 Agosti, 2026 jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi huo utakaohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wageni kutoka ndani na nje ya nchi, wananchi na wadau wa maendeleo.
” Uzinduzi huu wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ni tukio la kihistoria na hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kujenga mfumo wa nishati ya uhakika nchini, sambamba na kuchochea shughuli za uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, huu ni mradi mkubwa Zaidi wa kuzalisha umeme kuwahi kutekelezwa nchini kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiwa na uwekezaji wa takribani Shilingi trilioni 7.452.” Amesema Mhe. Ndejembi
Akifafanua kuhusu mradi huo, amesema JNHPP imeendelea kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia katika Gridi ya Taifa na hivyo kusaidia kupunguza changamoto za upungufu wa uzalishaji zilizokuwa zikichangia mgao wa umeme nchini, ambapo hadi tarehe 31 Mei 2026, kituo hicho kilikuwa kimezalisha takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja Hivyo kituo hicho kimekuwa kikichangia takribani nusu ya umeme wote unaotumika nchini Tanzania.
Kuhusu gharama za mradi huo, Mhe. Ndejembi amesema fedha iliyotumika kujenga mradi huo ni takriban dola za Marekani Bilioni 3.35 sawa na Shilingi za Tanzania Trilioni 7.452 ambapo pamoja na mradi huo kukusudiwa kuzalisha umeme, utasaidia pia kwenye kudhibiti mafuriko katika mto Rufiji, kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya binadamu.
Ameeleza kuwa ujenzi wa mradi wa JNHPP ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025 ambapo uwezo wa Bwawa la kutunza maji ni Mita za ujazo Bilioni 33 (Takribani mara 10 ya Bwawa la Mtera). Bwawa hili ni ziwa la kujenga na linashika nafasi ya nne kwa ukubwa katika maziwa yaliyoko nchini (Baada ya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa) huku kituo cha kuzalisha umeme cha JNHPP kinashika nafasi ya nne kwa ukubwa katika bara la Afrika.
Ameongeza kuwa uwekezaji wa JNHPP unaendana moja kwa moja na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo mradi huo ni sehemu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha Gridi ya Taifa na kuweka mazingira bora kwa uchumi kukua kwa kasi.
Katika mkutano huo Waziri Ndejembi amewaalika Watanzania wote kufuatilia na kushiriki katika tukio hilo ambalo ni kielelezo cha mafanikio makubwa katika historia ya sekta ya nishati na maendeleo ya Taifa.



