Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Watu saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa tuhuma za kuiba magari mawili yaliyotolewa bandarini na kupelekwa bandari kavu (ICD) Vingunguti na kubadili mwelekeo kwenda Kigamboni.
Magari hayo mawili yalitolewa bandarini kuelekea bandari kavu (ICD) Vingunguti, Dar es Salaam, yamedaiwa kubadilishiwa mwelekeo na kupelekwa Kigamboni, jambo lililozua wasiwasi kwa wahusika.
Washitakiwa hao ni Isack Gerald Natus, Samson Mwamoto, Daniel Noah, Adam Sufian, Michael Wambura Marwa, Fadhil Arumia Munisi na Tusho Kalambire ambapo walisomewa mashtaka.
Wote saba wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Victoria Mwaikambo, na kusomewa shtaka hilo ambapo wote wamekana.
Akisoma maelezo ya shtaka, Wakili wa Serikali, Nicas Kihemba, amedai kuwa washitakiwa hao waliiba magari mawili moja aina ya Nissan Caravan na lingine Toyota Regiusace yaliyokuwa yametolewa bandarini kwa ajili ya kupelekwa ICD Vingunguti mali ya Sudais Logistic Company Limited.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, badala ya magari hayo kufikishwa katika ICD yalipokuwa yakipelekwa, mwelekeo wake ulibadilishwa na kupelekwa Kigamboni.
Imedaiwa kuwa Agosti 12, 2026, operesheni maalumu ya kudhibiti wizi wa magari na vifaa vinavyotolewa bandarini kwenda ICD mbalimbali iliwafikisha maofisa katika nyumba ya Michael Wambura, ambako magari hayo mawili yalikutwa.
Kukamatwa kwa magari hayo kulisababisha washitakiwa saba kutiwa mbaroni kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Washitakiwa wote walikana shtaka hilo ambapo upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa kesi hiyo itaendelea katika hatua nyingine za kisheria.
Hakimu Mwaikambo ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, 2026, itakapotajwa tena. Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana.








