Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
DODOMA. Safari ya takribani miaka nane ya Serikali kujenga Mji wa Serikali Mtumba imefikia hatua ya kihistoria, huku Serikali ikitangaza kukamilika kwa sehemu kubwa ya miundombinu ya eneo hilo na maandalizi ya uzinduzi rasmi wa majengo ya Wizara, taasisi za Serikali na mtandao wa barabara za lami yakikamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kukamilika kwa Mji wa Serikali Mtumba ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu yenye miundombinu inayokidhi mahitaji ya shughuli za Serikali za kisasa.
Amesema hatua hiyo inafikia kilele Septemba 8, 2026, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo ya Wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa jumla ya kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba.
Prof.Kabudi amesema uzinduzi huo utafanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya shughuli zinazolenga kuonesha hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa eneo hilo ambalo sasa limegeuka kuwa kitovu muhimu cha shughuli za Serikali jijini Dodoma.
“Kukamilika kwa majengo hayo kutatoa mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi kwa jumla ya watumishi 18,510, hatua inayoonesha ukubwa wa uwekezaji uliofanyika na nafasi ya Mji wa Serikali katika kuboresha mazingira ya utendaji wa Serikali,”amesema.
MWANZO WA SAFARI YA MIAKA NANE
Akizungumzia mwanzoni wa Mji wa Serikali Mtumba Prof.Kabudi amesema haukujengwa kwa siku moja na kwamba Safari yake ilianza mwaka 2018, wakati Serikali ilipoanza kutekeleza hatua za awali za kujenga mazingira ya kuwezesha Wizara na taasisi za Serikali kufanya kazi Dodoma.
Hatua ya kwanza ya ujenzi ilianza Novemba 28, 2018, kwa kujenga majengo 23 ya muda kwa ajili ya ofisi za Serikali. Majengo hayo yalikamilika Machi 22, 2019, na kuwezesha baadhi ya Wizara na taasisi kuanza kuhamia eneo hilo.
Katika hatua hiyo pia zilijengwa ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na jengo la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua iliyoweka msingi wa kuanza kwa shughuli za Serikali Mtumba wakati maandalizi ya ujenzi wa majengo ya kudumu yakiendelea.
“Huo ukawa mwanzo wa safari ya kuligeuza eneo la Mtumba kutoka eneo la ujenzi wa majengo ya Serikali na kuwa mji maalumu wenye mifumo ya barabara, maji, umeme, mawasiliano, TEHAMA, usalama na huduma nyingine muhimu,”amesisitiza
AWAMU YA PILI YAPELEKA MTUMBA KIWANGO KINGINE
Kuhusu awamu ya pili amesema hatua kubwa zaidi ilifikiwa Oktoba 2021, Serikali ilipoanza awamu ya pili ya ujenzi iliyolenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya Wizara na taasisi mbalimbali.
“Tofauti na awamu ya kwanza iliyolenga kuweka mazingira ya awali ya kuanza kwa shughuli za Serikali, awamu ya pili imehusisha ujenzi wa miundombinu ya kudumu na mifumo mbalimbali inayolenga kuufanya Mji wa Serikali kuwa eneo kamili la shughuli za Serikali,”amesema.
Amesema Miongoni mwa miundombinu hiyo ni barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1, miundombinu ya mawasiliano, Uwanja wa Mashujaa pamoja na mifumo mbalimbali ya huduma za msingi.
Aidha, ujenzi umehusisha miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42, mifumo ya maji safi na maji taka, TEHAMA, kamera za usalama (CCTV), kituo cha zimamoto pamoja na upandaji miti na uboreshaji wa mandhari.
Kwa mantiki hiyo, Mji wa Serikali Mtumba haukujengwa kama mkusanyiko wa majengo ya ofisi pekee, bali kama mfumo mpana wa miundombinu unaolenga kuwezesha Serikali kufanya kazi katika mazingira ya kisasa, salama na yenye huduma zinazounganishwa.
WATUMISHI 18,510 KUPATA MAZINGIRA MAPYA YA KAZI
Moja ya mambo makubwa yanayoifanya awamu hii kuwa ya kipekee ni uwezo wa majengo mapya kuhudumia watumishi 18,510.
Prof.Kabudi amesema majengo hayo yameundwa kwa kuzingatia mahitaji na ukubwa wa Wizara na taasisi husika, kupitia mifumo minne ya usanifu.
Ametaja Mfumo wa kwanza kuwa umeundwa kuchukua hadi watumishi 300, wakati wa pili una uwezo wa kuchukua hadi 500.
“Mfumo wa tatu ndiyo mkubwa zaidi ukiwa na uwezo wa kuchukua hadi watumishi 1,400, huku mfumo wa nne ukiwa umeandaliwa kwa taasisi zenye wastani wa watumishi 150,Mpangilio huo unaonesha kuwa Serikali imezingatia tofauti za ukubwa na mahitaji ya taasisi katika kupanga matumizi ya majengo hayo,”amesema.
WATAALAMU NA WAKANDARASI WA NDANI WASHIRIKI
Katika utekelezaji wa awamu ya pili,Waziri huyo amefafanua kuwa Serikali pia imeendelea kutumia uwezo wa ndani kupitia taasisi zake pamoja na kampuni za ndani za sekta binafsi.
Amesema Jumla ya wakandarasi 11 wamehusika katika ujenzi wa majengo ya Wizara na taasisi, ambapo watano ni taasisi za Serikali na sita ni kampuni kutoka sekta binafsi.
Aidha, washauri elekezi watano waliotumika wote ni taasisi za Serikali.
Amezitaja Taasisi hizo ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Ushauri ya Chuo Kikuu Ardhi (ABECC), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Kampuni ya Watumishi Housing Investment.
Ushiriki huo unaonesha nafasi ya wataalamu na taasisi za ndani katika kubuni, kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa.
MTUMBA KUELEKEA KUWA ‘MJI JANJA’
Katika usanifu wa majengo na miundombinu ya awamu ya pili, Serikali imezingatia dhana ya mji wa kisasa unaokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na utunzaji wa mazingira.
“Dhana ya ‘smart city’ au mji janja imepewa nafasi, sambamba na dhana ya mji wa kijani, matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, uzingatiaji wa Sheria za Mipango Miji, Mpango Kabambe wa Mji wa Serikali pamoja na tathmini ya athari kwa mazingira,”amesema Waziri Kabudi.
“Uwekezaji wa Mtumba haujajikita katika kujenga ofisi pekee, bali umeelekezwa pia katika kujenga mazingira endelevu yatakayoweza kukidhi mahitaji ya Serikali kwa miaka ijayo,”ameeleza
TAASISI MBALIMBALI ZA SERIKALI ZAHUSIKA
Ujenzi wa miundombinu ya Mji wa Serikali umehusisha taasisi mbalimbali kulingana na majukumu yao.
TARURA imehusika na ujenzi wa barabara na miundombinu yake, wakati Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imehusika na mifumo ya maji safi na maji taka.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limehusika na miundombinu ya umeme, huku Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) likihusika na mifumo ya mawasiliano.
Waziri huyo amesema Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umehusika na usimikaji wa mifumo ya kamera za usalama, huku Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ikihusika na mifumo ya TEHAMA na uunganishaji wa majengo katika mifumo hiyo.
“Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limehusika na mfumo wa gesi asilia, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likihusika na huduma za zimamoto na uokoaji, huku Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ukihusika na upandaji miti na ustawishaji wa mandhari,”ameeleza.
BARABARA 57.1KM ZAFUNGUA MTUMBA
Mbali na majengo ya Wizara na taasisi, mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 57.1 ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayotarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia.
Barabara hizo zitawezesha usafiri ndani ya Mji wa Serikali na kurahisisha ufikaji wa watumishi, wageni na wananchi katika maeneo mbalimbali ya huduma.
Mtandao huo pia unaunganisha majengo na maeneo mbalimbali ya Mji wa Serikali, hivyo kuufanya Mtumba kufanya kazi kama eneo moja lenye mifumo ya miundombinu inayounganika.
SAMANI ZAKAMILISHA MAZINGIRA YA KAZI
Prof.Kabudi amesema Katika kuhakikisha majengo yanaanza kutumika yakiwa tayari kwa shughuli za Serikali, hatua nyingine iliyotekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa samani katika ofisi za Wizara 26 na taasisi zitakazotumia majengo hayo.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwekezaji wa majengo unaenda sambamba na maandalizi ya mazingira ya kazi, badala ya kukamilisha majengo pekee na kuacha hatua nyingine za matumizi zikiwa hazijakamilika.
MTUMBA, ALAMA YA DODOMA YA SERIKALI
“Kwa miaka kadhaa, Dodoma imeendelea kubeba jukumu la kuwa kitovu cha shughuli za Serikali baada ya uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali jijini humo,
Katika muktadha huo, Mji wa Serikali Mtumba umeendelea kuwa miongoni mwa alama kubwa za utekelezaji wa azma hiyo,”ameeleza.
Amefafanua kuwa Ujenzi wa majengo ya Wizara, taasisi, barabara na miundombinu mingine umeongeza shughuli za Serikali katika eneo hilo na kwa upande mwingine kuchochea mahitaji ya huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.
Kwa Dodoma, maendeleo ya Mtumba yana maana zaidi ya majengo ya Serikali. Yanaongeza fursa za biashara, usafirishaji, huduma za chakula, makazi, usalama na huduma nyingine zinazotokana na ongezeko la shughuli na watu.
SEPTEMBA 8, UKURASA MPYA
Septemba 8, 2026, Rais Samia anapotarajiwa kuzindua majengo ya Wizara 26, taasisi 11, barabara za lami na miundombinu mingine iliyokamilika, tukio hilo litakuwa kilele cha safari iliyoanza takribani miaka nane iliyopita.
Safari hiyo ilianza na majengo ya muda mwaka 2018, ikaingia katika ujenzi wa majengo ya kudumu mwaka 2021 na sasa kufikia hatua ambayo maelfu ya watumishi wataweza kufanya kazi katika mazingira mapya ya Mji wa Serikali Mtumba.
“Kwa hiyo, uzinduzi wa Mtumba si tukio la kukata utepe pekee,ni hatua inayobeba historia ya utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu chaSafari ya miaka nane ya Mji wa Serikali yafikia kilele: Rais Samia kuuzindua Septemba 8 shughuli za Serikali, huku ikiweka msingi wa utendaji wa Serikali unaotegemea majengo ya kisasa, teknolojia, miundombinu bora na mazingira endelevu,”amesema.
Mtumba sasa ni zaidi ya majengo ya Serikali,ni sura ya Dodoma mpya ya Serikali, alama ya uwekezaji wa taifa na sehemu ya historia ya utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”ameeleza Prof.Kabudi
Mwisho





