Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, amewakaribisha wawekezaji na taasisi za fedha za kimataifa kutumia fursa pana za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, hususan katika sekta za nishati, miundombinu na uzalishaji viwandani.

Mhe. Balozi Yakubu alitoa wito huo tarehe 9 Septemba 2026, jijini Paris, wakati akichangia katika Mkutano wa Kundi la Marafiki wa Afrika katika Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), uliojadili namna ya kuimarisha upatikanaji wa fedha na uwekezaji kwa ajili ya mageuzi ya uchumi wa Afrika.

Katika mchango wake, Mhe. Balozi alieleza kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6, ukichagizwa na sera bora za uchumi na uwekezaji pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 100 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025.

Aidha, alieleza kuwa Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja na taifa lenye ushindani, ubunifu, viwanda imara na matumizi endelevu ya rasilimali zake.

Mhe. Balozi Yakubu pia ameipongeza OECD kwa kuanzisha Jukwaa la Uwekezaji la Afrika kwa Njia ya Mtandao—Africa Virtual Investment Platform (AVIP)—litakalosaidia kuongeza uwazi wa taarifa, kuunganisha miradi na wawekezaji na kuhamasisha mitaji binafsi kuelekezwa katika miradi ya maendeleo barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi 16 za awali zinazoshiriki katika jukwaa hilo.

Alihitimisha kwa kutoa wito kwa OECD na washirika wa Afrika kuendelea kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, masoko ya mitaji na majukwaa ya taarifa ili fursa na uwezo mkubwa wa uwekezaji wa Tanzania na Afrika kwa ujumla uweze kutambulika na kutumiwa kikamilifu.