Na Dk Reuben Lumbagala

Michezo ni sekta muhimu inayotoa ajira kwa vijana wengi duniani. Kutokana na hilo, mipango madhubuti huwekwa ili kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia michezo na kuchangia maendeleo ya nchi.

Tanzania si kisiwa. Kwa namna michezo ilivyobadili hali za maisha za watu wengi, hatuna budi kuipa msukuma sekta hiyo muhimu ili vijana wengi waweze kupata kipato.

Mbunge wa Jimbo la Pangani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameipa kipaumbele sekta ya michezo Jimboni kwake.

Aidha, amedhamiria kutumia michezo kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zinazopatikana wilayani Pangani ili wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wazitumie katika kukuza maendeleo.

Kwa miaka mingi, Aweso amekuwa mfadhili wa mashindano mbalimbali ya michezo ili kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.

Mei 16, 2026, Aweso alikuwa Mgeni Rasmi wa fainali ya mashindano ya Aweso Vijana Cup, yaliyoratibiwa na Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo huku yeye akiwa mfadhili wake.

Katika siku hiyo, Aweso alisema mashindano hayo ni rasharasha, anakuja na mashindano makubwa ya “Aweso Cup 2026,” ambayo washindi wataibuka na zawadi nono.

“Kwa kuwa mimi ni mdau wa michezo, mashindano yajayo ya Aweso Cup 2026, mshindi wa kwanza atajinyakulia shilingi milioni kumi, wapili milioni tano na watatu milioni tatu,” amesema Aweso.

Ni faraja kuona, miezi mitatu tangu atoe ahadi hiyo, ametimiza kwa kuanzisha mashindano hayo huku washindi wakitarajiwa kuibuka na zawadi hizo alizoahidi. Mashindano hayo yanachagizwa na kaulimbiu isemayo “Wekeza Pangani.”

Kimsingi, kamati ya mashindano hayo imeshakamilisha mchakato wa kanuni na ratiba, ambapo timu 80 zinatarajiwa kushiriki huku ufunguzi rasmi ukitarajiwa kufanyika Septemba 12, 2026, katika uwanja wa Casablanca, Sakura.

Pamoja na burudani ya michezo, vijana kutoka timu 80 zinazoshiriki mashindano hayo, wana fursa ya kuonyesha vipaji vyao ili kujipatia kipato.

Aidha, fursa za uwekezaji kama uvuvi, uchumi wa buluu, utalii, biashara, ufugaji, kilimo, huduma za jamii, kutaja kwa uchache, zinatarajiwa kunadiwa kupitia mashindano hayo. Hakika Aweso Cup 2026, Wekeza Pangani – ni daraja la kukuza vipaji, uchumi na maendeleo.