Na Dk Reubeni Lumbagala, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha wanawapatia huduma bora na kwa urahisi kule walipo.
Katika kutekeleza hilo, Februari 25, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar, akishirikiana na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Mwenda, walizindua ofisi zinazotembea (mobile offices) Jijini Dar es Salaam ambazo ni magari yenye maofisa wa TRA na vifaa vya kazi, tayari kwa kuwahudumia wananchi.
Kupitia ofisi hizo zinazotembea, maofisa hao wamekuwa wakiwafikia wateja na wananchi kwa kuwapa elimu na ushauri wa masuala ya kodi. Pia kufanya usajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Huduma nyingine ni kupata leseni za udereva, kutoa makadirio na namba za malipo ya kodi. Pia, wananchi wanapata elimu na ufafanuzi kuhusiana na mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi yaliyofanyika katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Kimsingi, ofisi hizo zimekuwa na manufaa kwani zinawafikia wananchi kule walipo na kwa urahisi. Huduma ambazo zinatolewa katika ofisi za TRA zinapatikana katika magari tembezi.
Ikumbukwe kuwa, mkakati wa TRA ni kuongeza wigo wa walipakodi ili kuongeza mapato. Katika mazingira haya ya kuwafikia wananchi kupitia ofisi tembezi, idadi ya walipakodi nchini itaongezeka.
TRA imebeba dhima kubwa ya kutimiza malengo ya serikali ya kukuza maendeleo kupitia ukusanyaji kodi. Na ukusanyaji kodi unategemea uhusiano mzuri uliopo baina ya Mamlaka hiyo na walipakodi nchini.
Hivyo basi, ofisi zinazotembea zinachangia uboreshaji wa uhusiano huo kwa kuwafuata walipakodi kule walipo. Jambo la kuzingatia ni walipakodi na wananchi wazitumia ofisi hizo ili kupata elimu ya kodi na masuala mengine mengi kwa ajili ya kukuza maendeleo ya nchi yetu kupitia ulipaji kodi wa hiari


