Na Zawadi Msalla

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ipo mbioni kuzindua mwongozo wa tathmini ya misingi ya utawala nchini.

Mwongozo huo umelenga kuangalia hali ya uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora na kuweka mfumo unaoweza kutumika kupima namna taasisi za umma, binafsi na mifumo ya utawala inavyotekeleza misingi ya utawala bora.

Mwongozo huo pia imelenga kuwa nyenzo muhimu katika kubaini mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zilizopo na maeneo yanayohitaji maboresho katika nyanja ya utawala bora.

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia rasimu hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Jijini Dodoma leo, Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Bi. Suzan Ndeona amesema kazi ya uandaaji wa nyaraka hiyo muhimu kwa nchi, ilianza rasmi mwaka 2023 kwa kuangalia vigezo mbalimbali na uhitaji wa nchi wa kuwepo mwongozo na nyenzo itakayotumika katika kufanya tathmini ya Utawala Bora nchini.

Bi. Suzan amesema mwongozo huo umeweka vigezo vyote muhimu vya upimaji wa uwepo wa utawala bora katika Taasisi. Aidha ameeleza mwongozo huo utaendelea kuboreshwa ili kuhakikisha unaenda sambamba na mabadiliko mbalimbali ya kimfumo yanayoendelea nchini kama vile upimaji wa Watumishi wa Umma (PEPMIS).

“Bado mwongozo huu ni rasimu, utakapokamilika utawekwa mezani kupata maoni ya taasisi za umma, binafsi, na mashirika mbalimbali ambayo yanahusika na masuala ya utawala bora”. Amesema Bi. Suzan.

Miongoni mwa misingi muhimu itakayoangaliwa na kufanyiwa tathimini ni pamoja na uwazi, uwajibikaji, usawa, utawala wa sheria, ushirikishwaji, ufanisi na tija, maridhiano, mwitikio na uadilifu.

Akieleza kuhusu misingi ya utawala bora, Bi. Suzan alisema misingi hiyo ina uhusiano wa moja kwa moja na jamii kwa kuwa utawala bora huonekana kupitia taasisi zinavyotoa huduma, kusikiliza wananchi, kutumia rasilimali na kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria.

Naye Bi Hellen Siriwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wakati wa kutoa wasilisho la rasimu hiyo, amesema NBS imeshirikiana kikamilifu na THBUB katika kuandaa nyenzo za kufanyia tathmini kwa kuangalia namna ambavyo nchi itafaidika na mwongozo huo ulioandaliwa. Aliongeza kuwa NBS itaendelea kushirikiana na THBUB katika kuhakikisha kuwa mwongozo huo unakamilika na kuweza kuzinduliwa rasmi Kitaifa.

Mwongozo huo utakuwa nyenzo ya kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika taasisi za umma na binafsi kwa kutambua mapema maeneo yenye changamoto na kuchukua hatua za maboresho kabla ya kutokea kwa madhara.