Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema mkoa umeziagiza wilaya na halmashauri kuandaa na kutenga maeneo maalumu yatakayotumika kuwahifadhi wananchi watakaokumbwa na mafuriko yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha Oktoba mwaka huu.
Aidha Nyongo ametoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyowahi kukumbwa na mafuriko, hususan baadhi ya maeneo ya Rufiji, Delta , Rufiji na Kibiti pamoja na wanaoishi mabondeni, kuchukua tahadhari mapema na kuondoka katika maeneo hatarishi kabla ya mafuriko kutokea.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ,mjini Kibaha septemba 16,2026 kuhusu maandalizi ya Mkoa kukabiliana na mvua hizo, Nyongo alisema wananchi wanapaswa kutambua maeneo yatakayotengwa na wilaya kwa ajili ya hifadhi endapo mafuriko yatatokea.
Alieleza kupitia timu ya maafa, mkoa umetambua maeneo mbalimbali yaliyo katika hatari ya mafuriko, yakiwemo Delta ya Rufiji na maeneo ya Ruvu, huku wataalamu wakiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema.
Nyongo aliwataka wananchi kuanza kuweka akiba ya dawa, maji na vyakula kwa matumizi ya dharura, akieleza kuwa mafuriko yanaweza pia kuathiri mitambo na mabomba ya maji, hivyo kuwa na akiba ya maji kutasaidia wakati wa dharura.
Kadhalika mkoa umejipanga kwa vifaa vya dharura na mifumo ya mawasiliano itakayosaidia kurejesha mawasiliano endapo yatakatika, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapoona maeneo hatarishi.
Alisema maandalizi mengine yaliyofanywa na mkoa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano, ufuatiliaji, maandalizi na mwitikio wa haraka, huku akizitaka halmashauri na wananchi kushirikiana kusafisha mifereji ya maji na maeneo yanayoweza kuziba na kusababisha maji kutuama.





