Sheria kuanzisha Bodi ya Wajiolojia kusimamia na kuratibu taaluma nchini
Serikali kutenga asilimia 10 ya mapato ya madini kwa utafiti wa jiosayansi
Taarifa sahihi za jiolojia kuimarisha uwekezaji na kuwalinda wadau wa madini
Na Mwamdishi Wetu
Wizara ya Madini imewasilisha pendekezo la kuanzishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Wajiolojia nchini katika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, hatua inayolenga kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia taaluma hiyo na kuhakikisha taarifa za jiosayansi zinazotolewa nchini zinakuwa sahihi na zenye kuaminika.
Hayo yamebainishwa leo, Septemba 16, 2026, jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS).
Dkt. Kiruswa amesema endapo Sheria hiyo itapitishwa, itaanzishwa Bodi ya Wajiolojia itakayokuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuimarisha taaluma hiyo, ikiwemo kuweka viwango vya kitaaluma na kuhakikisha wataalamu wanaohusika na shughuli za jiosayansi wanatambulika na kuwajibika ipasavyo.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na umuhimu wa taarifa za jiosayansi katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uwekezaji katika sekta ya madini, huku akieleza kuwa kumekuwa na baadhi ya taarifa zisizo sahihi zinazotolewa na watu wasio waaminifu au wasiokuwa na weledi na ujuzi unaohitajika, hali ambayo imekuwa ikisababisha hasara kwa baadhi ya wadau wa sekta hiyo.
“Ni muhimu kuwa na chombo kitakachosimamia taaluma hii ili kuhakikisha taarifa za jiosayansi zinazotokana na tafiti zinazofanywa nchini zinakuwa za uhakika na zinatolewa na wataalamu wenye sifa, weledi na uwajibikaji,” amesema Dkt. Kiruswa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amesema Serikali imefanya uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na mapato yasiyo ya kodi katika sekta ya madini kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini nchini, ambapo fedha hizo zinakadiriwa kufikia takribani Sh bilioni 140.
Amesema fedha hizo zitawezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuongeza kasi ya tafiti za jiosayansi na kuzalisha taarifa nyingi na sahihi zitakazosaidia kubainisha rasilimali zilizopo nchini na kuweka msingi imara wa uwekezaji katika sekta ya madini.
Dkt. Kiruswa amesema Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania katika kuimarisha taaluma hiyo na kuhakikisha wataalamu wa ndani wanashiriki kikamilifu katika tafiti na shughuli za jiosayansi zinazolenga kuongeza manufaa ya rasilimali za madini kwa Taifa.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inakwenda sambamba na vipaumbele vya Wizara vinavyotokana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Sera ya Madini, ambavyo ni pamoja na kuongeza utafiti na upatikanaji wa taarifa sahihi za jiolojia, kuongeza thamani madini, kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi, kurasimisha na kuboresha uchimbaji mdogo, pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania, Prof. Alisante Mshiu, amesema Mkutano Mkuu wa Mwaka ulianza Septemba 14, 2026, ukiwa na dhima ya “Matumizi ya Suluhisho za Jiosayansi kwa Ukuaji wa Viwanda, Uhakika wa Upatikanaji wa Nishati, Kuelekea Matumizi ya Nishati Safi na Maendeleo Stahimilivu Tanzania.”
Amesema mkutano huo umelenga kutoa fursa kwa wataalamu kubadilishana uzoefu na maarifa katika nyanja mbalimbali za jiosayansi, kwa lengo la kuongeza matumizi ya taaluma hiyo katika kutatua changamoto za maendeleo, kukuza uchumi na kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali zilizopo nchini.








