Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Benki ya NMB imesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa ndani katika kuimarisha utawala bora, usimamizi wa vihatarishi na kujenga imani ya wadau, hususan wakati huu ambapo taasisi zinakabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia, vihatarishi vinavyobadilika na matarajio yanayoongezeka kutoka kwa wadau.

Akizungumza katika Kongamano la 13 la Utawala Bora na Kongamano la 19 la Mwaka la Wakaguzi wa Ndani nchini yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, alisema nafasi ya wakaguzi wa ndani imeendelea kuwa muhimu katika kusaidia taasisi kufanya maamuzi sahihi na kujenga mifumo imara ya utawala.

Baragomwa aliyasema hayo wakati Benki ya NMB ikishiriki na kudhamini makongamano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) kuanzia Septemba 21 hadi 25, 2026, yakilenga pamoja na mambo mengine kuimarisha nafasi ya wakaguzi wa ndani katika kutoa maarifa, kuchochea ubunifu na kujenga uaminifu ndani ya taasisi.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais – Ikulu Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, aliipongeza NMB kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha utawala bora nchini kupitia udhamini na ushiriki wake katika makongamano hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Eng. Kenneth Nindie, alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali inatambua umuhimu wa wakaguzi wa ndani katika kuimarisha utendaji na utawala bora wa taasisi.

Ushiriki wa NMB katika makongamano hayo ulienda zaidi ya udhamini, ambapo viongozi waandamizi wa Benki pia walishiriki katika mijadala ya kitaalamu kwa kuwasilisha mada zinazohusu maeneo muhimu ya uendeshaji na utawala wa taasisi. Mkurugenzi wa Uhusiano wa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Innocent Yonazi, aliwasilisha mada kuhusu uendelevu pamoja na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG) na Mkurugenzi wa Bodi na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori, aliwasilisha mada yenye Kichwa “Trust: The Currency of Internal Audit”