Na Mwandishi Wetu, JamuhuriMedia, Songea

Makanisa ya Kipentekoste mkoani Ruvuma yameandaa tamasha kubwa la nyimbo za injili kwa lengo la kuliombea Taifa, kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Watanzania.

Tamasha hilo la siku Tatu limeanza Novemba 13, 2026, katika Viwanja vya Mashujaa, vilivyopo Manispaa ya Songea, likiwakutanisha waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, wakiwemo Maaskofu, Wachungaji ,viongozi wa makanisa, waimbaji wa nyimbo za injili pamoja na wananchi walioshiriki katika tukio hilo la kiroho.

Akizungumza na waandishi wa habari Jana Novemba 13, 2026 katika viwanja vya mashujaa, Mratibu wa tamasha la nyimbo za Injiri na Maombezi ya Kitaifa, Mchungaji Yusto Chanangula, amesema kuwa lengo kuu ni kuwakutanisha watu wa Mungu katika kuliombea Taifa kupitia nyimbo za injili na maombi, huku akisisitiza umuhimu wa amani na umoja nchini.

Amesema kuwa kanisa lina nafasi kubwa katika jamii, siyo tu katika kufundisha neno la Mungu, bali pia kuhamasisha upendo, mshikamano na maadili mema kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Kupitia tamasha hilo, waimbaji mbalimbali walipata nafasi ya kuimba nyimbo za injili zilizobeba ujumbe wa kumtukuza Mungu, kuhimiza imani na kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kumtegemea Mungu katika maisha yao.

Aidha, tamasha hilo limekuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa makanisa ya Kipentekoste na kuonesha namna muziki wa injili unavyoweza kutumika kama nyenzo ya kuunganisha jamii na kuhamasisha maombi ya pamoja kwa ajili ya Taifa.