SERIKALI imesema itaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda haki, usalama na ustawi wa watu wenye ualbino, huku ikisisitiza umuhimu wa kuwapa fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Palamagamba Kabudi, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino.
Amesema mpango huo umeandaliwa kwa lengo la kuweka mfumo jumuishi wa kulinda na kukuza haki na ustawi wa watu wenye ualbino, ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama, kuzuia ubaguzi, unyanyasaji na ukatili pamoja na kuhakikisha wanapata huduma na fursa sawa katika nyanja mbalimbali za maisha.
Kabudi amesema Serikali pia imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino, wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Ametaja hatua hizo kuwa ni kutenga rasilimali kwa ajili ya upatikanaji wa mafuta kinga dhidi ya mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino ili kuzuia madhara ya mionzi hiyo na saratani ya ngozi.
Hatua nyingine, amesema, ni kuimarisha huduma za afya na miundombinu inayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, kuanzisha na kuimarisha vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani pamoja na kuendelea kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu watu wenye ulemavu.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kupitia madawati ya jinsia na watoto ndani ya Jeshi la Polisi.
Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa kielektroniki wa taarifa za watu wenye ulemavu unaofika hadi ngazi za vijiji na mitaa ili kuwezesha Serikali kupanga na kutoa huduma kwa usahihi.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia fursa za mikopo yenye masharti nafuu zinazotolewa na Serikali na mamlaka za Serikali za mitaa.
Akizungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Kabudi amesema lengo ni kujenga Taifa ambalo kila Mtanzania, bila ubaguzi, atakuwa na uwezo, ujuzi na fursa za kushiriki katika maendeleo na kufurahia maisha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Africa Albinism Network, Martin Haule, amesema jukwaa hilo ni muhimu si kwa Tanzania pekee bali pia kwa Bara la Afrika, kutokana na changamoto zinazowakabili watu wenye ualbino katika nchi mbalimbali.
Amesema changamoto hizo ni pamoja na unyanyapaa, ubaguzi, ukosefu wa fursa sawa katika elimu na ajira, pamoja na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya, ulinzi na haki.
Haule amesema uzoefu unaonyesha kuwa mabadiliko chanya yanawezekana pale watu wenye ualbino wanaposhirikishwa kikamilifu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maamuzi yanayowahusu.
Amepongeza Tanzania kwa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Watu wenye Ualbino kupitia nguzo zake za kinga, ulinzi, uwajibikaji na usawa pamoja na kutobagua.
Amesema anatarajia majadiliano ya siku nne ya jukwaa hilo yatazaa matokeo, majukumu yaliyo wazi, mifumo imara ya upatikanaji wa rasilimali na ramani ya utekelezaji itakayosaidia kulinda na kuendeleza haki za watu wenye ualbino hadi mwaka 2029 na kuendelea.
“Mapambano ya watu wenye ualbino si suala la kundi moja pekee, ni suala la haki za binadamu, utu, usawa na maendeleo jumuishi kwa wote,” amesema.




