*Bei yapanda karibu asilimia 51 kutoka Wazo Hill hadi Ubungo, umbali wa kilomita 22 tu
*Yagonga ongezeko la asilimia 131 maduka ya rejereja jijini Dar es Salaam
Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mfuko wa saruji unaondoka kiwandani Wazo Hill, Tegeta jijini Dar es Salaam, ukiuzwa Sh 11,227. Unafika kwa wakala mkuu, Ubungo, umbali wa kilomita 22 tu, bei inakuwa Sh 16,940.
Ndani ya safari hiyo fupi, bei inaongezeka kwa Sh 5,713, sawa na asilimia 50.9.
Hapo ni Ubungo. Mfuko unapofika ‘site’ kuuzwa rejareja, mnunuzi anakutana na bei kati ya Sh 21,000, sawa na ongezeko la asilimia 87 kutoka bei ya kiwandani, hadi Sh 26,000 — ongezeko la asilimia 131 katika baadhi ya maeneo.
Butiama mkoani Mara, JAMHURI limethibitisha mfuko mmoja kuuzwa hadi Sh 30,000.
Ni nini kimesababisha mtafaruku huu katika mnyororo wa thamani ya mfuko wa saruji?
Kwa upande wa viwanda, tatizo linaelekezwa zaidi kwenye klinka; malighafi muhimu katika uzalishaji wa saruji, matengenezo ya mitambo, ongezeko la ghafla la mahitaji na gharama za usafirishaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Portland Cement Public Limited (TPCPLC), Alfonso Velez, ameliambia JAMHURI kuwa kampuni haikuongeza bei ya kiwandani wakati soko lilipokumbwa na upungufu wa saruji.
TPCPLC ndiyo inayozalisha saruji ya chapa ya Twiga katika kiwanda chake cha Wazo Hill, Dar es Salaam.
Velez pia anazungumzia mwenendo wa Tanga Cement Public Limited (TCPLC), inayozalisha saruji ya chapa ya Simba katika kiwanda cha Pongwe, Tanga. Kampuni hizo mbili ni viwanda tofauti vilivyo chini ya mmiliki mmoja.
“Nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa mbaya kutokana na mvua pamoja na mahitaji hafifu ya saruji. Ghafla, mwishoni mwa Julai 2026 mauzo yaliongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Tuliombwa kuuza ndani ya mwezi mmoja kiwango cha saruji ambacho kwa kawaida tungeuza ndani ya miezi minne,” amesema Velez.
Mahitaji yaliporuka, uzalishaji wa klinka ukakumbwa na changamoto. Mitambo inayozalisha malighafi hiyo huhitaji matengenezo, huku baadhi ya wazalishaji wakikabiliwa na changamoto za uzalishaji wakati mahitaji yakiongezeka.
“Wakati huo, baadhi ya viwanda vya klinka vilikumbwa na changamoto za uzalishaji. Gharama za usafirishaji pia ziliathiriwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta,” amesema Velez.
Kwa habari za kina zaidi soma Gazeti la Jamhuri la Septemba 29- Oktoba 5, 2026



