*Wagonjwa wahaha kusaka dawa nje ya hospitali, vifaa tiba vya zaidi ya Sh 300 milioni navyo vyakwama kwa hadi miaka 10
*Mashine muhimu za uchunguzi zakosa wataalamu, wananchi walazimika kusaka huduma kwingine
*Ripoti ya JAMHURI yawagusa wahitimu wa vyuo, wasema wako tayari kufanya kazi kwa kujitolea
Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Liwale
Mgonjwa anaandikiwa dawa hospitalini. Anapofika dirishani anaambiwa haipo, analazimika kuitafuta kwenye duka binafsi.
Nyuma ya hali hiyo, maswali yanaibuka. Wilayani Liwale, dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 404 zimekwisha muda wa matumizi; pembeni kuna vifaa tiba vya zaidi ya Sh milioni 300vimeharibika, kuondolewa katika matumizi au kusubiri hatua nyingine, baadhi vikikaa kwa kati ya miaka saba hadi 10.
Kwingineko kuna mashine muhimu za uchunguzi ambazo matumizi yake yanaathiriwa na ukosefu wa wataalamu.
Cha kushangaza, nje ya Liwale wapo wataalamu waliosomea kazi hizo ambao hawana ajira; na baada ya kusoma ripoti ya JAMHURI kuhusu hali hiyo, baadhi yao sasa wamejitokeza wakisema wako tayari kwenda kufanya kazi kwa kujitolea wakisubiri ajira.
Kuna wahusika walifanya hali hii kuwa ni siri?
Dawa, vifaa tiba na miundombinu ya huduma za afya ni fedha za walipa kodi wa Tanzania wanaohitaji huduma, inasikitisha zinaposhindwa kutumika kwa wakati.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa dawa zilizokwisha muda Liwale si tatizo lililoanza jana.
Mfamasia wa Wilaya, Steven Lutego, amesema dawa hizo zimekuwapo katika taarifa za serikali kwa zaidi ya miaka minne, huku hatua za kuziondoa zikisubiri kukamilika kwa taratibu za kisheria na kiutawala.
Anasema tatizo haliishii kwenye dawa pekee. Wilaya pia ina mzigo wa vifaa tiba vilivyoharibika, vilivyopitwa na wakati au ambavyo havikidhi viwango vinavyohitajika kwa matumizi ya wagonjwa.
Baadhi vinasubiri kibali cha kuteketezwa, vingine kufanyiwa ukarabati au uamuzi wa namna ya kuviondoa katika matumizi.
Miongoni mwa vifaa vilivyotajwa ni mashine za kupimia shinikizo la damu, viti vya meno, mizani, vitanda vya kujifungulia na mashine nyingine kadhaa.
Baadhi ya vifaa hivyo, kwa mujibu wa Lutego, vimekaa kwa zaidi ya miaka saba hadi 10.
“Baadhi ya ‘delivery bed’ zimeondolewa kwenye matumizi baada ya kubainika hazikuwa salama kwa wajawazito, huku vifaa vingine vikiwa vimekaa muda mrefu bila kutumika,” amesema. Baadhi ya vifaa hivyo vimehifadhiwa katika eneo la hospitali baada ya kuondolewa katika matumizi, jambo ambalo Lutego amesema si salama kimazingira na kunaongeza uwezekano wa maeneo hayo kuwa mazalia ya wadudu na wanyama waharibifu.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA SEPTEMBA 29 – HADI OKTOBA 5, 2026




