Na Mwadishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) , David Kafulila, amesema ubia kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kusaidia mashirika ya umma kukabiliana na changamoto za mtaji, ubunifu na ufanisi wa usimamizi katika utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma.

Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Wenyeviti wa bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum ) 2026 unaofanyika jijini Arusha .

Amesema kazi kubwa ya kituo hicho ni kusaidia sekta binafsi kuingia katika mikataba ya muda mrefu na mamlaka za Serikali ili kushirikiana katika kutekeleza miradi ambayo kwa kawaida ingetekelezwa na Serikali, lakini inaweza kufanyika kwa kutumia mitaji na utaalamu wa sekta binafsi.

Kafulila amesema ubia huo unalenga kuleta mambo matatu muhimu, ambayo ni mtaji kutoka sekta binafsi, ubunifu pamoja na mifumo bora ya usimamizi na ufanisi wa kiutendaji, hivyo kusaidia Serikali kutekeleza majukumu yake bila kutegemea fedha za umma pekee.

Amesema changamoto za upatikanaji wa mitaji, ubunifu na ufanisi wa usimamizi ni miongoni mwa sababu zinazofanya mashirika ya umma kuhitaji fursa za kushirikiana na sekta binafsi, huku akisisitiza kuwa mikutano inayowakutanisha wadau inalenga kutafuta majawabu ya changamoto hizo.

Kafulila ameongeza kuwa, katika uendeshaji wa mashirika ya umma kuna mazingira yanayohitaji kuangaliwa kwa kina wakati wa kupima ufanisi, kwa kuwa Serikali wakati huo huo inaweza kuwa mtunga sera, mmiliki, mtoa fedha na mdhibiti wa shirika husika.

Amesema kwa mfano, mashirika kama TANESCO, TRC na MSD yanamilikiwa na Serikali, huku Serikali ikiwa pia na jukumu la kuyasimamia kupitia wizara husika, kuyapatia fedha na kuweka mifumo ya udhibiti wa huduma wanazotoa.

Kafulila amefafanua kuwa, changamoto hiyo inaongezeka pale mashirika yanapotoa huduma kwa taasisi nyingine za Serikali, kwa kuwa mteja na mmiliki wa huduma hiyo anaweza kuwa Serikali hiyo hiyo, kama ilivyo kwa huduma za maji na umeme zinazotolewa katika shule, taasisi, majeshi na polisi.

Amesema hali hiyo inaweza kuathiri uwezo wa shirika kuonyesha ufanisi wa kibiashara, hasa pale linapoelekezwa kutoa bidhaa au huduma kwa bei ambayo si ya soko, jambo linaloweza kusababisha hasara ambayo baadaye hutafsiriwa kama udhaifu wa uendeshaji.

“Unakuta kuna hasara ambazo zimetengenezwa na bei za maelekezo, lakini kwa upande mwingine unasema shirika ni bovu, halina ufanisi. Kumbe sababu kubwa ni kwamba limeuza bidhaa zake kwa bei isiyo ya soko,” amesema Kafulila.

Amesema katika kupima utendaji wa mashirika ya umma, ni muhimu kuzingatia mazingira na majukumu yaliyopewa mashirika hayo badala ya kuangalia hasara au faida pekee, ili kutofautisha changamoto zinazotokana na uendeshaji na zile zinazotokana na maamuzi au maelekezo ya Serikali.

Kafulila amesema Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwaandaa vijana kwa kuwapa nafasi za mafunzo kwa vitendo katika mashirika ya umma, akieleza kuwa mpango wa kuwaingiza vijana 10,000 katika taasisi hizo unaweza kuwasaidia kupata uzoefu na kuwaandaa kwa majukumu ya baadaye.

Amefafanua kuwa, sambamba na kuwekeza katika rasilimali watu, mashirika yanapaswa kuangalia kwa umakini matumizi yake, ikiwemo gharama za vikao vya bodi na shughuli nyingine zinazoweza kufanyika kwa gharama kubwa, ili fedha zitumike katika maeneo yenye tija na hatimaye kuongeza ufanisi wa mashirika ya umma.