Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pemba
Mwakilishi wa Jimbo la Wingwi, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kombo Mwinyi Shehe, amekabidhi mota yenye thamani ya Shilingi milioni 8.5 kwa ajili ya kusaidia usambazaji wa maji katika Kijiji cha Sizini na maeneo jirani.
Tukio hilo limefanyika leo, Septemba 30, 2026, katika Kijiji cha Suzini, ambapo mota hiyo imekabidhiwa kwa wananchi wa eneo hilo pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).
Akikabidhi mota hiyo, Mwakilishi Kombo Mwinyi Shehe amesema kero ya maji katika kijiji hicho ilikuwa ikimnyima usingizi kutokana na hali ngumu iliyokuwa ikiwakabili wananchi.
“Leo Alhamdulillah, sasa naweza kupata usingizi. Tatizo la maji tumelishughulikia na tumeliweka sawa,” alisema Shehe.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona changamoto mbalimbali katika jamii, ili ziweze kushughulikiwa kabla hazijawa kubwa na kuwa ngumu kutatuliwa.
Kijiji cha Suzini kilikabiliwa na ukosefu wa maji kwa zaidi ya siku tano baada ya mota iliyokuwa ikitumika kusukuma maji kuungua na kushindwa kufanya kazi.
Kukabidhiwa kwa mota hiyo kunatarajiwa kusaidia kurejesha huduma ya maji kwa wananchi wa Suzini na maeneo jirani.
Kwa upande wake, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wananchi wa Suzini, Khamisi Shehe Maalim, amempongeza Mwakilishi Kombo Mwinyi Shehe kwa kuthamini na kuchukua hatua za kutatua kero hiyo.
“Alhamdulillah, amesikia kilio chetu na tunamshukuru Mwakilishi kwa kuitatua kero ambayo ilikuwa ngumu kustahimili,” alisema Maalim.





