Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Deogratias Sangu, ameitaka Tume ya Madini kuimarisha mikakati ya kuitangaza tanzanite katika masoko ya kimataifa, akisema madini hayo ni miongoni mwa alama muhimu zinazoitambulisha Tanzania duniani.

Dkt. Sangu ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili mkoani Geita.

Amesema tanzanite ina umuhimu wa kipekee kwa Tanzania kwa kuwa hupatikana katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, eneo linalotajwa kuwa chanzo pekee kinachojulikana duniani cha madini hayo.

Aidha, Dkt. Sangu ameipongeza Tume ya Madini kwa usimamizi wa Sekta ya Madini, akisema juhudi hizo zimechangia mafanikio mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuimarika kwa ushiriki wa Watanzania na wawekezaji kutoka nje katika sekta hiyo, pamoja na kupungua kwa vitendo vya utoroshaji wa madini.

Maonesho hayo ya kitaifa yanaendelea kwa lengo la kutoa fursa kwa wadau kujifunza kuhusu teknolojia, uwekezaji, uzalishaji, uongezaji thamani na biashara ya madini, na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3, 2026