Na Mwandishi Wetu, Jamuhuri Media,Songea

SHULE ya Sekondari Ruhuwiko inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita, hali inayodhihirisha juhudi za shule hiyo katika kukuza taaluma.

Hayo yameelezwa na mkuu wa shule hiyo Luteni Kanali Benedicto Bahame kwenye mahafari ya 3 ya kidato cha nne na Darasa la saba ambayo yamefanyika Jana katika viwanja vya shule hiyo, alisema kuwa Matokeo hayo yameendelea kuifanya Ruhuwiko kuwa miongoni mwa shule zinazotajwa kwa kufanya vizuri kitaaluma katika Mkoa wa Ruvuma.

Kwa mujibu wa taarifa za matokeo ya mitihani ya kitaifa, wanafunzi wa shule hiyo wameendelea kupata matokeo mazuri katika mitihani ya Kidato cha Nne na Sita, wakionesha uwezo katika masomo mbalimbali ambapo mwaka Jana shule ilishika nafasi ya Tisa kitaifa kwa wahitimu wa kidato cha sita.

Luteni Kanali Bahame alisema Mafanikio hayo yameelezwa kuwa yanatokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kujifunzia, nidhamu ya wanafunzi, kujituma kwa walimu pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya wanafunzi.

Aidha mkuu huyo wa shule Luteni Kanali Bahame alieleza kuwa shule hiyo itaendelea kuweka mkazo katika kuongeza ufaulu na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayowawezesha kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wanafunzi wameeleza kuwa nidhamu, kujisomea kwa bidii, ushirikiano kati yao na walimu pamoja na programu mbalimbali za kitaaluma vimekuwa sehemu ya mafanikio yao.

Kwa upande wake mgeni rasmi Brigedia Jenerali Sijaona Myala Kamanda wa Brigedi ya Kusini ameupongeza uongozi wa shule kwa mafanikio hayo huku akiwahusia wahitimu kuendeleza nidhamu,utii, na uzalendo kwa Nchi yao pindi watakapokuwa uraiani.

Aidha, Brigedia Jenerali Myala amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kulipa ada kwa wakati ili kuwezesha shule kutekeleza mipango yake ya maendeleo na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza ufaulu zaidi.

Luteni Kanali Benedicto Bahame Mkuu wa shule ya Sekondari Ruhuwiko.