Na Mwandishi wetu, Geita

WAZIRI wa Madini Anthony Peter Mavunde kwenye maonyesho ya tisa ya teknolojia ya madini yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan Manispaa ya Geita amemkabidhi gari mdau wa madini Jofrey Mwaselela ambaye amenunua gari hilo kupitia kampuni ya GF Trucks.

Mchimbaji madini huyo Mwaselela aliyekabidhiwa funguo ya gari hilo na Waziri Mavunde amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine kwa kuwa yanawawezesha kupata bidhaa na huduma zinazohitajika karibu na maeneo yao ya shughuli.

Mwaselela amesema awali baadhi ya wachimbaji walilazimika kusafiri hadi viwandani kutafuta vifaa na mashine, ila kupitia maonesho hayo wamekuwa wakipata fursa ya kuona na kununua bidhaa hizo moja kwa moja.

“Ushirikiano wetu sisi AMOTEC na GF Trucks umekuwa ukitusaidia kupata vifaa na huduma zinazohitajika katika shughuli zetu za uchimbaji wa madini,” amesema Mwaselela.

Meneja chapa na masoko wa kampuni ya GF Trucks, Smart Deus amesema kampuni hiyo imepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wachimbaji, huku baadhi yao wakifanya manunuzi na wengine kuonyesha nia ya kununua bidhaa na vifaa vinavyotolewa na kampuni hiyo.

“Kupitia maonyesho haya tumepata mzigo mkubwa wa mauzo, na jumamosi ya Oktoba 3, mwaka 2026 tunakwenda kumkabidhi mteja wetu mkubwa ambaye amechukua zaidi ya magari 10,” amesema Smart.

Amesema mwitikio huo umeendelea kuipa kampuni hiyo hamasa ya kushiriki maonyesho hayo, ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka tisa, kutokana na mahitaji makubwa ya magari na vifaa kutoka kwa wachimbaji.

“GF Trucks imekuwa ikichangia katika utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani kupitia kiwanda chake cha kuunganisha magari, kinacholenga kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini,” amesema Smart.

Amesema uwepo wa kiwanda hicho unalenga kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kwenda sambamba na kasi ya Serikali katika kukuza maudhui ya ndani katika sekta ya madini.

Amesema GF Trucks pia imeungana na taasisi mbalimbali za fedha ambazo zimekuwa chachu ya biashara katika maonesho hayo kwa kuwezesha wateja kupata huduma za kifedha zinazowasaidia kufanya manunuzi.