Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kasulu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameendelea na ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji ambapo ametembelea eneo la mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la Kasulu Sugar, wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusisitiza umuhimu wa ardhi iliyotolewa kwa uwekezaji kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema, Serikali inataka kuona maeneo yote yaliyotolewa kwa wawekezaji yakiendelezwa na kuleta tija kwa mujibu wa makubaliano na mipango iliyowekwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo mwenye dhamana ya kuunda Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi ya uwekezaji ambapo mbali na jukumu hilo pia kamati inamshauri Kamishna wa Ardhi katika kushughulikia maombi ya umilikishaji ardhi.
Dkt. Akwilapo amefanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki katika eneo la mradi huo linalomilikiwa na kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar, lenye ukubwa wa hekta 37,662.
“Wizara haitarajii kuona ardhi inayotolewa kwa ajili ya uwekezaji ikiendelea kubaki bila kuendelezwa”.amesema Mhe Dkt Akwilapo.
“Kuendelezwa kwa eneo hili kutasaidia kuongeza uzalishaji miwa na sukari, kupanua upatikanaji wa bidhaa hiyo sokoni na kuwa na mchango katika kupunguza changamoto ya bei ya sukari nchini”. Ameeleza.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Mufindi Papers Mills Co. Limited Bw. Satya Narayana amemueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, mradi unaotekelezwa na kampuni yake unatumia teknolojia ya hali ya juu na ya kisasa katika uzalishaji sukari.
“Mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari katika kiwanda hiki unagharimu dola 320 milioni na unatarajia kuchangia uchumi wa Tanzania na jamii kwa ujumla”. Amesma.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na jitihada za kufuatilia matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya uwekezaji kwa lengo la kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa tija, kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na masharti yaliyowekwa.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuhakikisha wawekezaji wanatimiza wajibu wao na kuongeza mchango wa uwekezaji katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.











