Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
JUMLA ya wanafunzi 4,213,144 wamesajiliwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, Darasa la Nne na Kidato cha Pili utakaofanyika mwezi huu Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 4, 2026, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026 katika shule za msingi 21,008.
Amesema jumla ya wanafunzi 1,591,064 wamesajiliwa kufanya upimaji huo, ambapo wavulana ni 764,284 sawa na asilimia 48.04 na wasichana 826,780 sawa na asilimia 51.96.
“Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika tarehe 05 Oktoba, 2026 hadi tarehe 6 Oktoba, 2026 katika jumla ya Shule za Msingi 21,008 Tanzania Bara,” amesema Profesa Mohamed.
Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026 katika shule za msingi 21,353, ambapo wanafunzi 1,827,367 wamesajiliwa.
Kati yao, wavulana ni 906,545 sawa na asilimia 49.61, huku wasichana wakiwa 920,822 sawa na asilimia 50.39.
Profesa Mohamed amesema kati ya wanafunzi hao, 1,675,355 sawa na asilimia 91.68 watafanya upimaji kwa lugha ya Kiswahili, huku 152,012 sawa na asilimia 8.32 wakifanya kwa lugha ya Kiingereza kulingana na lugha wanayotumia katika kujifunza.
Kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Darasa la Pili, amesema jumla yao ni 5,295, wakiwemo 1,062 wenye uoni hafifu, 112 wasioona, 929 wenye uziwi, 1,208 wenye ulemavu wa akili na 1,984 wenye ulemavu wa viungo.
Kwa Darasa la Nne, amesema wanafunzi 5,603 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa, wakiwemo 1,282 wenye uoni hafifu, 105 wasioona, 957 wenye uziwi, 1,378 wenye ulemavu wa akili na 1,881 wenye ulemavu wa viungo.
Akizungumzia Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, Profesa Mohamed amesema utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026, katika shule za sekondari 6,612 Tanzania Bara pamoja na vituo 599 vya watahiniwa wa kujitegemea Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema jumla ya wanafunzi 794,713 wamesajiliwa, ambapo wanafunzi wa shule ni 786,163 na watahiniwa wa kujitegemea ni 8,550.
“Kati ya wanafunzi wa Shule 786,163 waliosajiliwa, wavulana ni 351,536 sawa na asilimia 44.72 na wasichana ni 434,627 sawa na asilimia 55.28,” amesema.
Amesema wanafunzi 781,127 watafanya upimaji katika Mkondo wa Jumla kwa mara ya kwanza, kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, huku wanafunzi 5,036 wakifanya upimaji katika Mkondo wa Amali.
Profesa Mohamed amesema maandalizi ya upimaji huo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa karatasi za upimaji na nyaraka muhimu katika Halmashauri na Manispaa zote nchini, pamoja na maandalizi maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Amesema Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu, huku mazingira ya vituo vya upimaji yakiandaliwa ili kuwa salama na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.
Aidha, amewataka wasimamizi wa upimaji kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia Kanuni za Mitihani, huku wakihakikisha wanafunzi wote wanafanya upimaji katika hali ya utulivu na kupata haki zao.
NECTA imewaonya wanafunzi dhidi ya vitendo vya udanganyifu, ikisema mwanafunzi yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani.
Wamiliki na wakuu wa shule wametakiwa kutoingilia majukumu ya wasimamizi wa upimaji, huku Baraza likionya kuwa kituo kinaweza kufutwa endapo usalama wa upimaji utahatarishwa.


