Na OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kufanya kazi usiku na mchana ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kuwanufaisha wananchi kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño zinazotarajiwa, kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Prof. Shemdoe ametoa agizo hilo Oktoba 3, 2026, wakati wa kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza miradi ya TACTIC, Wakandarasi, Wahandisi Washauri, Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA pamoja na Waratibu wa Miradi ya TACTIC wa Halmashauri.
“Wakandarasi nendeni mkafanye kazi usiku na mchana ili kama mvua za El Niño zikija, zikute mmeshakamilisha miradi yote na hatimaye wananchi wanufaike kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewaelekeza wakandarasi wote waliopo kazini kuondoa vifusi kwa wakati kando ya mifereji wa barabara, vilivyotokana zoezi la kuzibua mifereji ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhali dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, ili vifusi hivyo visirejeshwe tena na maji ya mvua kwenye mifereji ya barabara.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka Wakandarasi kuwasilisha kwa Wahandisi Washauri mipango kazi mipya ya utekelezaji wa miradi hiyo, ambapo Wahandisi hao wataijadili pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kabla ya kuiwasilisha kwake kupitia kwa wataalamu wa OWM–TAMISEMI kwa ajili ya kuipitia na kuipitisha ili itumike katika ufuatiliaji wa utekelezaji.
Prof. Shemdoe amewashauri Wakandarasi ambao utekelezaji wa miradi yao uko chini ya kiwango kuhakikisha wanatoa mikataba midogo (sub-contract) kwa Wakandarasi wengine wenye uwezo wa kukamilisha kazi kwa wakati, ili miradi hiyo iweze kuendelea na kukamilika kwa mujibu wa mikataba. Amesema hatua hiyo itawawezesha kuwasilisha hati za madai ya malipo kwa mwajiri na kupata fedha zitakazowawezesha kukamilisha miradi, akieleza kuwa Mhe. Rais tayari amewezesha upatikanaji wa fedha za malipo kwa Wakandarasi.
Katika kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi, Prof. Shemdoe amesema ameunda Minister’s Delivery Team, Timu ya Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Maelekezo yake itakayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa OWM–TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu kwa ajili ya ufuatiliaji wa Miradi ya barabara za TARURA, na kuongeza kuwa itakuwa ikifuatilia kila siku utekelezaji wa miradi na kuwasilisha kwake taarifa kila baada ya wiki mbili, hatua inayolenga kutekeleza azma ya Mhe. Rais ya kuwaunganisha Watanzania kupitia mtandao wa barabara.
Ili kujenga uelewa kuhusu sababu za marekesho ya wigo wa utekelezaji wa miradi (rescoping), Prof. Shemdoe amewaelekeza washitiri kufanya vikao vya kujenga uelewa kwa wadau wote wenye nafasi ya kuusemea mradi wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wa maeneo husika, Viongozi wa Chama, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri au Meya wa Manispaa husika.
Katika hatua ya kuhakikisha maelekezo hayo yanafuatiliwa na kutekelezwa, Prof. Shemdoe ameelekeza kikao kazi kingine kifanyike baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa, huku akitarajia kwamba ifikapo wakati wa kikao kazi hicho, kila Mkandarasi atakuwa amefikia hatua nzuri katika utekelezaji wa miradi ya TACTIC, na hatimaye wananchi waanze kunufaika na miundombinu inayojengwa katika maeneo yao.











