Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ametoa rai kwa mamlaka za miji, taasisi na wananchi kuanza kuchukua hatua za maandalizi dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño na kusisitiza umuhimu wa upangaji bora wa maeneo ya makazi na uimarishaji miundombinu.

Dkt. Akwilapo ametoa rai hiyo Oktoba 5, 2026 jijjni Dodoma wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026, yaliyofanyika chini ya kaulimbiu isemayo Makazi Toshelezi kwa Wote.

Amesema, uzoefu wa mafuriko yaliyowahi kutokea nchini ni ukumbusho wa umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kulinda maisha ya wananchi, makazi na miundombinu.

“Tusisubiri mvua inyeshe ndipo tuanze kuchukua hatua, kila mmoja wetu aanze sasa. Mamlaka za miji na taasisi zote zizingatie hatua zote kama zilivyoelekezwa na mamlaka za nchi ili kupunguza athari za janga hili,” amesema Dkt. Akwilapo.

Akizungumzia makazi bora, Dkt. Akwilapo amesema, makazi toshelezi hayamaanishi kuwa na nyumba pekee, bali yanahusisha nyumba salama, ardhi iliyopangwa, huduma muhimu, usalama wa miliki, miundombinu imara pamoja na mazingira yanayoweza kustahimili changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, amesema ongezeko la watu na kasi ya upanuzi wa miji nchini linahitaji mipango madhubuti ya kuhakikisha maeneo ya makazi yanapangwa na kuendelezwa kwa kuzingatia usalama wa wananchi na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, ikiwemo mafuriko.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha maendeleo ya makazi na miji, ikiwemo mchakato wa maboresho ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji na changamoto za Tanzania ya sasa.

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, juhudi za Serikali katika kuboresha miji zinaenda sambamba na utekelezaji Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Ajenda Mpya ya Miji na Lengo la 11 la Maendeleo Endelevu (SDG 11), linalolenga miji na makazi kuwa jumuishi, salama, himilivu na endelevu.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratias Kalimenze akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga ameielezea Siku ya Makazi Duniani kuwa inatoa fursa ya kutafakari kwa pamoja kuhusu hali ya makazi nchini, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora salama na ya gharama nafuu.

Kwa upande wake Mwakilishi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani nchini Tanzania Dkt. Grace Lubaale amesema wakati dunia ikiadhimisha siku ya Makazi duniani Tanzania inaendelea kukua kwa kasi huku miji nayo ikiendelea kupanuka.

“Ukuaji huu unaongeza mahitaji ya nyumba, ardhi iliyopangwa, miundombinu na huduma za msingi, hivyo tunahitaji kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali katika kutafuta kwa pamoja suluhisho kwa pamoja “kidole kimoja hakivunji chawa”amesema.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila mwaka Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ambapo kwa mwaka huu wa 2026 siku hiyo imeadhimishwa Oktoba 5, 2026.