Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA) inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha miundombinu ya barabara na kuendelea kuziboresha ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za El Nino.

Jitihada hizo zimebainishwa na Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Namtumbo Mhandisi Albert Mtimba amebainisha kuwa moja ya kazi zinazofanyika ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Muungano lenye urefu wa mita 30 linalotarajiwa kukamilika na kuanza kutumika ifikapo tarehe 28 Novemba, 2026.

“Mradi huu wa ujenzi wa Daraja la Muungano ni muhimu sana kwa wananchi kwani kipindi cha masika huwa ni vigumu kuvuka upande wa pili kwani mto unajaa maji lakini pia kuna mamba katika mto huu.” Amesema Mhandisi Albert.

Aidha, amefafanua kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutasaidia wananchi kusafirisha mazo yao kwenda sokoni, usafiri wa kwenda katika Hospitali ya Wilaya lakini pia watoto wataweza kwenda shuleni kwa urahisi.

Naye, Bi. Sifa Seleman mkazi wa Namtumbo amesema kuwa huduma za afya hasa kwa mama na mtoto huwa ngumu kipindi cha masika kutokana na kukosa daraja.

“Mradi huu utatusaidia hasa sisi akina mama kwani kuna wakati watu hulazimika kujifungua katika mazingira hatarishi”. Amesema Bi. Sifa.

Pia, Bw. Amir Simba ambaye ni mkazi wa Namtumbo ameipongeza serikali kupitia TARURA kwa utekelezaji wa mradi huo ambao ni mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kote nchini ikiwemo ujenzi wa vivuko na barabara ili kuwawezesha wananchi kutekeleza shughuli zao mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii.